Mahakama Yatupa Pingamizi la mke wa Bilionea Msuya..Adai Aliteswa Sana



Dar es Saalaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali pingamizi la mke wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini, marehemu Erasto Msuya ‘Bilionea Msuya’, Miriam Mrita aliyekuwa akipinga maelezo yake ya onyo kupokewa katika kesi ya mauaji inayomkabili.

Hivyo, mahakama imepokea maelezo hayo na kuwa kielelezo cha kwanza cha ushahidi wa upande wa mashtaka, baada ya kujiridhisha kuwa yalichukuliwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria.

Jaji Edwin Kakolaki alifikia hatua hiyo jana baada ya kutupilia mbali hoja zote tatu za mshtakiwa huyo zilizotolewa na wakili wake na kukubaliana na hoja za upande wa mashtaka kuwa maelezo hayo yalichukuliwa kwa kufuata matakwa ya sheria.

Uamuzi huo unatokana na kesi ndogo iliyoibuka ndani ya kesi ya msingi baada ya upande wa mashtaka kupitia shahidi wake wa kwanza kuiomba mahakama iyapokee maelezo hayo kuwa sehemu ya ushahidi wa shahidi wa kwanza na pia kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.


Miriam anakabiliwa na kesi ya mauaji ya wifi yake, Aneth Msuya, pamoja na mwenzake, mfanyabiashara Revocatus Muyella. Wanadaiwa kumuua Aneth nyumbani kwake, maeneo ya Kibada Kigamboni, Dar es Salaam, Mei 25, 2016.

Kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018 iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi na upande wa mashtaka wakati shahidi wa kwanza, WP 4707 Sajenti Mwajuma (42), aliyeandika maelezo uliomba mahakama iyapokee yawe sehemu ya ushahidi wake na kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Awali, wakili wa utetezi, Peter Kibatala alipinga kupokewa kwa maelezo hayo akitoa sababu tatu ikiwemo kuteswa, akidai hakuyatoa kwa hiari yake, bali ilitokana na mateso kutoka kwa askari Polisi.


Pia alidai maelezo hayo yalichukuliwa nje ya muda wa saa nne zinazoelekezwa kwa mujibu wa sheria, baada ya kutiwa mbaroni. Pia hakupewa haki zake za msingi wakati wa kuandika maelezo hayo.

Kutokana na pingamizi hilo, Jaji Kakolaki alilazimika kusimamisha kesi ya msingi na kusikiliza kwanza kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, ili kujiridhisha na uhalali wa uchukuaji maelezo hayo kama umekidhi matakwa ya kisheria.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili mwandamizi, Erick Tesha akishirikiana na Gloria Mwenda na Caroline Matemo uliwaita mashahidi watatu akiwemo WP 4707 Sajenti Mwajuma, aliyeandika maelezo hayo ambaye pia shahidi wa kwanza katika kesi ya msingi. Upande wa utetezi pia uliwaita mashahidi watatu akiwemo mshtakiwa wa kwanza mwenyewe, Miriam na mdogo wake, Mbaazi Mrita pamoja na askari wa magereza ambaye ni daktari wa zahanati ya gereza la Segerea, Pembe Zuberi.

Akitoa uamuzi wake jana, Jaji Kakolaki alisema mahakama imeona madai yaliyotolewa na Mrita hayana msingi, kwani mshtakiwa alifahamishwa wakati akichukuliwa maelezo yake.


Jaji Kakolaki pia alisema hoja kwamba maelezo yalichukuliwa nje ya muda wa saa nne hayana msingi kwa sababu mshtakiwa alikamatwa Agosti 5, 2016 saa 11 jioni na alipelekwa kituo kikuu cha polisi Arusha na baada ya kufika kituoni hapo walimsubiri Mkuu wa Upelelezi mkoa (RCO) ambaye alifika saa 2 usiku na kuondoka naye hadi nyumbani kwake walikofanya upekuzi kuanzia saa 5 usiku hadi saa 11 alfajiri Agosti 6, 2016.

“Agosti 6, 2016 walienda kwenye hoteli ya mshtakiwa huyo kuangalia magari yanayosadikika yalitumika kwenye tukio hilo na kisha alisafirishwa kuja Dar es Salaam ambapo alifika usiku sana wakalazimika kulala kutokana na uchovu waliokuwa nao,” alisema Jaji Kakolaki akirejea ushahidi wa upande wa mashtaka na kuongeza:

“Hayo yote yalifanywa chini ya ulinzi wa polisi, hivyo maelezo yake yalichukuliwa Agosti 7, 2016 ambayo yalikuwa ndani ya muda kwa kuwa alihojiwa kuanzia saa 3:30 asubuhi hadi saa 7:30 mchana.” Kuhusu hoja ya kuteswa, Jaji Kakolaki alisema haina mashiko kwa sababu haibishaniwi kuwa maelezo yake yalichukuliwa Agosti 7, 2016 kuanzia saa 3:30 asubuhi hadi saa 7:30, lakini ndio muda anaodai kuwa aliteswa.

Kuhusu hoja ya mshtakiwa huyo kuwa na kidonda mguuni kilichofanya mguu kuvimba kwa madai ya kutokana na mateso aliyoyapata, Jaji Kakolaki alisema hakuna uthibitisho unaoonyesha alipigwa na alikuwa kwenye hali mbaya.


“Hivyo mahakama hii imetupilia mbali hoja zote zilizotolewa na upande wa utetezi na imeamua kielelezo hicho kipokelewe,” alisema Jaji Kakolaki na kuamuru shahidi wa kwanza kuendelea na ushahidi wake.

Akifunga ushahidi wake, Ijumaa iliyopita, shahidi wa tatu wa upande wa utetezi katika kesi hiyo ndogo, Dk Zuberi aliieleza Agosti 24,2016 akiwa katika gereza la Segerea wakati akihakiki washtakiwa wapya waliofikishwa alimuona Mrita akiwa na kidonda ambacho hakijafanyiwa usafi kilichokuwepo juu ya mguu wake wa kushoto karibu na kidole cha mwisho, hivyo alimsafisha, kisha kumchoma sindano ya kutuliza maumivu na kuua bakteria.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad