Majaliwa ahoji kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kiberenge
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametaka wenye mawazo ya kuanzisha utaratibu wa kutumia viberenge kupanda Mlima wa Kilimanjaro wafikirie kwa kina jambo hilo na watoe maelezo ya kina kwa serikali.
Alitoa maagizo hayo jana wakati akifunga msimu wa 20 wa Kilimanjaro Marathon 2022 kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi.
Alisema anashangazwa na wenye mawazo ya kuanzisha viberenge vya kupandia Mlima Kilimanjaro kwani kufanya hivyo kutaondoa uhalisi wa kupanda mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika wenye urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari.
Watu wengi wanaupanda mlima huo kwa miguu kupitia njia ya Marangu yenye vituo vya Mandara, Horombo na Kibo, Gilmans na hatimaye kilele cha Uhuru.
Majaliwa alisema Mlima Kilimanjaro una heshima yake kwa mtu kuupanda mwenyewe mpaka juu bila ya kutumia vitu kama viberenge.
Alisema kitendo cha kuweka vyuma kwa kuchimbua chimbua ili kupitisha viberenge pia kutasababisha uharibifu wa uoto wa asili wa mlima huo na kumaliza theluji katika vilele chake.
Aliwataka waendelee kujadili jambo hilo lakini wahakikishe wanatoka na maelezo sahihi kwa serikali.
Majaliwa pia alihoji wapagazi wa mizigo kwa wanaopanda mlima huo watawapelekwa wapi kwa sababu watakosa ajira.
“Vikiwepo viberengo vya kupanda mlima wale watu wa kubeba mizigo hawatakuwepo, hivyo mtuambie wale watu mtawapeleka wapi?” alihoji huku akishangiliwa na umati.
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka watu kupanda kwa wingi miti ili kulinda theluji ya mlima huo kwani ni kivutio kikubwa cha watalii ambao wanaliingizia taifa pato kubwa.
Alizitaka mamlaka zinazohusika kuutangaza zaidi kimataifa utalii wa Tanzania na hasa Mlima Kilimanjaro na vivutio vingine ili watalii wengi zaidi watembelee nchini hasa wakati wa Kilimanjaro Marathon ambayo hufanyika kila mwaka.
Pia aliwataka wananchi kuendelea kuwa makini dhidi ya ugonjwa wa Covid- 19 na kutojiachia na badala yake waendelee kujitokeza kuchanja ili kujikinga na ugonjwa huo.
Pia aliwakumbusha wananchi kuhusu sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti mwaka huu nchini kote kuwa ni muhimu kwani itasaidia mambo mengi na kuwataka kutoa ushirikiano kwa wahusika.