KATIKA msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kumekuwa na wachezaji wengi vijana kutokana ndani na nje ya nchi.
Na hawapo tu mradi kujaza nafasi ya wachezaji 25 au 30 wanaoruhusiwa kusajiliwa, la hasha, badala yake kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakizisaidia timu zao zinazopambana kwenye ligi hiyo.
Ilikuwa ni mara chache sana kuona wachezaji vijana, hasa kwenye timu kubwa za Simba, Yanga na Azam, lakini msimu huu umeonekana ni wa mabadiliko.
Mbali na kuwa bado timu hizo zina wachezaji wakongwe, lakini vijana wameleta chachu kubwa, kwani si wale ambao wanaingia kipindi cha pili kwa sababu tu mchezaji fulani kachoka, ila wameonekana kuleta vitu tofauti na kuanza kuwa tegemeo, hawa ni wachache kati ya wengi walionyesha ubora na kutoa changamoto kubwa...
#1. Aboutwalib Mshery - Yanga
Ni golikipa wa Yanga ambaye amesajiliwa kipindi cha dirisha dogo akitokea Mtibwa Sugar. Ni kinda wa miaka 21 tu. Ni mmoja wa wachezaji vijana wanaofanya vema kwenye Ligi Kuu Tanzania mpaka sasa, akianzia na Mtibwa ambako amecheza nusu msimu kabla ya kuhamia Yanga.
Awali, mashabiki wa Yanga walikuwa na wasiwasi baada ya kipa namba moja Djigui Diarra kwenda kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Cameroon akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Mali.
Haraka wakamtwaa Mshery kuja kuchukua nafasi yake, na hadi sasa hajawaangusha. Amekuwa kwenye kiwango cha hali ya juu, kile kile ambacho alikuwa nacho Mtibwa Sugar.
#2. Tepsi Evans - Azam FC
Ana umri wa miaka 19 tu, lakini tayari ameshaanza kujichukulia umaarufu kwenye soka la Tanzania akiwa bado kinda kabisa. Ni mmoja wa wachezaji zao la Azam FC, akijiunga na 'akademi' hiyo mwaka 2016, lakini msimu huu anacheza Ligi Kuu.
Kwa nusu msimu tu, amekuwa moja ya wachezaji waliotia fora na kuvutia mashabiki wengi, akiwa anacheza kama kiungo mshambuliaji na pia winga. Hivi majuzi ameongezwa mkataba wa mwaka mmoja na timu yake, sasa utamalizika 2025, badala ya 2024.
#3. Peter Banda - Simba
Amesajiliwa msimu huu kutoka FC Shariff ya Moldovia, ambako alikuwa akicheza kwa mkopo, akitokea Nig Bullets ya Malawi.
Ingawa bado hajaonekana kupata nafasi sana kwenye kikosi cha Simba, lakini zile dakika chache anazoingia anaonekana ni mchezaji mwenye kipaji na hatari, ambaye anaweza kuibeba timu hiyo siku za usoni.
Ni suala la muda tu, pia anaweza kuipatia kipato klabu kwa kumuuza kwa klabu kubwa, kutokana na umri wake wa miaka 21 tu alionao. Banda, raia wa Malawi pia anaichezea timu ya taifa ya nchi yake na alicheza baadhi ya mechi kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) ambazo zilihitimishwa jana kwa Misri na Ivory Coast kucheza fainali jana.
#4. Denis Mkane - Yanga
Kinda huyu mwenye miaka 19, alisajiliwa na Yanga kipindi cha dirisha dogo la usajili msimu huu. Ni mmoja wa winga machachari ambaye hakukaa sana kwenye klabu yake ya Biashara United.
Achana na mechi ya kwanza dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara, lakini alifanya makubwa kwenye michuano ya awali ya Kombe la Shirikisho, akifunga bao moja kwenye moja ya mechi ya timu hiyo iliyochezwa,
kabla ya kujitoa yenyewe kwa kutokwenda kucheza mechi dhidi ya Al Ahly Tripoli ugenini. Akiwa Biashara United amefanya makubwa ikiwa ni pamoja na kupachika mabao.
Yanga imemsajili na kuonyesha uwezo mkubwa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, kabla ya kuwa majeruhi kwa sasa.
Hajacheza mechi yoyote ya ligi akiwa Yanga, lakini wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wana matarajio makubwa naye kutokana na umri wake, wakimfananisha na winga wa zamani wa timu hiyo, Mrisho Ngassa.
#5. Pachal Msindo - Azam
Huyu ni beki wa kushoto wa Azam FC ambaye naye amekuwa mmoja wa wachezaji wa kutegemewa msimu huu.
Pia naye amepandishwa kutoka chini kwenye 'akademi' ya alipojiunga mwaka 2016 kama Tepsi. Ni mmoja wa wachezaji ambao wanaonekana kuwa hazina kubwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars baadaye kama kiwango chake kitaendelea kuwa hivi. Ana miaka 18 tu.
#6. Israel Patrick - Simba
Anaichezea Simba na Timu ya Taifa, Taifa Stars. Ana umri wa miaka 21 sasa, na anaonekana ameanza kuaminika taratibu kwenye kikosi cha mabingwa hao.
Mwenda, ambaye ameshawahi kuzichezea klabu za Alliance, lakini Simba ikimsajili mwanzoni mwa msimu huu akitokea KMC.
Ana uwezo wa kucheza beki zote za pembeni, lakini wasichokijua wengi ni kwamba ana uwezo mkubwa wa kupiga vizuri penalti, na faulo, kiasi kwamba ameshawahi kuifungia Alliance mabao mengi, pamoja na bao moja Stars. Anaonekana anaweza kuwa mrithi sahihi wa Shomari Kapombe.