Dodoma. Mkutano wa sita wa Bunge umemalizika juzi jijini Dodoma, ukishuhudia mambo nane yaliyotikisa mijadala mbalimbali, likiwamo suala la kero ya ukatikaji umeme mara kwa mara.
Mengine ni mgogoro wa hifadhi ya Ngorongoro, mishahara hewa na kupitiwa kwa tozo ya miamala ya simu ili kuondoa manung’uniko ya wananchi.
Mambo mengine yaliyotikisa ni hoja kuhusu ucheleweshwaji wa miradi ya kimkakati, madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii, viashiria vya ubadhirifu katika Mamlaka ya Bandari (TPA) sambamba na mashirika kadhaa ya umma.
Tozo za simu
Akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo, mbunge wa kuteuliwa, Humprey Polepole alisema suala la tozo za miamala ya simu, halina budi kupelekwa bungeni kujadiliwa.
“Jambo limekuwa kubwa na lina interest (maslahi) kwa umma na limeleta manung’uniko kwa jamii. Serikali inafahamu linaweza kuwa jambo la kibajeti linagusa masuala ya kibajeti, linagusa mapesa ya Serikali, lakini umesikia hapo miamala imepungua,”alisema Polepole.
Hata hivyo, Serikali haikuwa na majibu ya moja kwa moja juu ya hoja hiyo.
Hofu kuchelewa kwa miradi
Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jerry Silaa alisema katika uchambuzi, kamati imebaini miradi mingi inayotekelezwa na mfuko wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), iko nje ya muda uliopangwa kukamilika kwake.
“Fedha zilizotumika kuwekeza katika miradi hiyo ni za wanachama, na zinapaswa kuwepo pindi zitakapohitajika kwa ajili ya kutekeleza jukumu lake kuu la kulipa mafao ya wanachama,”alisema Silaa.
Alisema kamati inalishauri shirika kuweka mkakati madhubuti wa kukamilisha miradi yake kwa muda uliopangwa, ili liweze kutimiza malengo ya uanzishwaji wa miradi hiyo.
Pia, kamati ilishauri shirika kufanya tathmini na kupitia upya maeneo ya uwekezaji ili kuhakikisha linawekeza katika maeneo yenye tija na yatakayolipatia shirika faida na kuongeza ajira kama vile kwenye viwanda.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Baran Sillo alisema kamati ilifanya uchambuzi wa barabara 38 zenye jumla ya kilomita 8,575.29 zilizopo kwenye hatua mbalimbali na kubaini kuwa kuna barabara ambazo zina miaka zaidi ya 10, lakini bado ziko kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na uchambuzi wa kina.
Alisema barabara mpya zinaendelea kuibuliwa, ilihali barabara za zamani hazijakamilika na kuna ongezeko la malipo ya riba kwa Serikali, inayotokana na kutolipwa kwa makandarasi kwa wakati kwa kigezo cha uhakiki.
Ukatikaji umeme
Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina alisema umefika wakati wa Bunge kuunda tume teule ya kibunge itakayochunguza na kubaini ukweli kuhusu ukatikaji umeme.
“Mnasema mitambo haikufanyiwa ukarabati kwa miaka sita, hebu tuambieni mbona wakati wote huo hakukuwa na katakata ya umeme, iweje leo msingizie hilo,” alihoji Mpina na kuwasihi kuacha kumhusisha Rais katika majibu yao aliyosema hayawasaidii Watanzania.
Akijibu hoja, Waziri wa Nishati, January Makamba aliwataka wabunge h kumpa muda wa kushughulikia changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
“Hii ni meli yetu wote, nikifeli mimi imefeli nchi, akifeli Rais imefeli nchi. Kama una matatizo na mheshimiwa Rais ama mimi kuwa waziri, tutafute jambo jingine sio mambo ya nchi,” alisema January.
Wabunge wengine waliochangia suala hilo ni Venant Protus (Igalula), Stella Manyanya (Nyasa), Jesca Kishoa (Viti Maalum) na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini Dustan Kitandula.
Ngorongoro moto
Baadhi ya wabunge waliochangia taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, waliibuka na sakata la wafugaji kuongezeka katika hifadhi ya Ngorongoro, jambo walilosema linatishia uhai wa hifadhi hiyo.
Hivyo, walishauri wafugaji hao waondolewe hifadhini, kwa kuwa baadhi yao wanatumika kuhudumia mifugo ya matajiri wasioishi eneo hilo.
Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga aliishauri Serikali iwaondoe kwa nguvu kwa Wamasai katika eneo hilo.
“Kama kule Mtwara wakati watu wanagoma gesi iondolewe mpaka wajue watafaidikaje, mlipeleka vifaru na vitu vingine kwamba iwe keki ya Taifa ili kila mmoja anufaike, tunaogopa nini? Au kwa sababu kuna matajiri? alihoji.
Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka aliyetetea kuwapo kwa wafugaji wa Kimasai.
“Wamasai hawa wamekuwa waungwana kwa uhifadhi. Kama kuna kabila lililoonyesha uhifadhi na kuishi na wanyama katika eneo moja bila kuwadhuru ni tarafa ya Ngorongoro, alisema Ole Sendeka.
Hata hivyo, akizungumza wakati wa kuahirisha Bunge juzi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema wananchi wanaoishi kwenye hifadhi ya Ngorongoro, watahama kwa hiyari yao .
Aliwataka wanaotaka kuhama kwa hiyari wajiorodheshe katika ofisi za wakuu wa wilaya za Ngorongoro na Karatu, ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha na kwa mhifadhi mkuu.
Majaliwa alisema Serikali inatambua kuhusu maisha ya watu wa huko, mifugo na mali nyingine, lakini inatambua pia kuwa uhifadhi nao ni muhimu kwa faida ya nchi.
Ubadhirifu Bandari
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilitaka kuwachukulia hatua watumishi wote wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) waliotajwa kushiriki mchakato wa ununuzi na usimikaji wa mfumo wa ununuzi na usimikaji (ERP), baada ya kusababisha hasara ya mabilioni ya fedha.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka alisema kutokamilika kwa mfumo huo, kumesababisha hasara kwa Serikali ya takribani Sh3.23 bilioni na Dola za Marekani milioni 2.30.
Viashiria vya mishahara hewa
Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), Mwenyekiti wa kamati hiyo Grace Tendegu, alisema kamati ilibaini viashiria vya kuibuka tena kwa mishahara hewa serikalini, baada ya kiasi cha mishahara kutoka Hazina kutofautiana na mahitaji halisi ya mishahara katika mfumo wa ‘Lawson’.
Alitoa mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ambapo mahitaji ya Lawson ilikuwa ni Sh13.16 bilioni, lakini Hazina ilitoa Sh13.30 bilioni na hivyo kusababisha ziada ya Sh145. 73 milioni.
Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mahitaji ya Lawson yalikuwa ni Sh17.67 bilioni, lakini Hazina ilipeleka Sh17.88 bilioni.