Marekani na washirika wake wamepambana na Urusi na China katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jana kuhusiana na umuhimu wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa na taathira zake katika nchi ambazo hivi sasa zimewekewa vikwazo kuanzia Korea Kaskazini, Yemen mpaka Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, pamoja na makundi ya al-Qaeda, dola la Kiislamu na washirika wao sambamba na wanaowaunga mkono.
Kiongozi wa masuala ya kisiasa katika Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo amesema vikwazo vya Umoja huo sio tena silaha yenye makali kama ilivyokuwa.
Tangu mwaka 1990 yamefanyika mabadiliko ya kupunguza uwezekano wa vikwazo kuwaathiri raia na nchi za ulimwengu wa tatu na kwa hivyo baraza la usalama la Umoja huo limejumuisha mabadiliko hayo na matokeo yake kuziondolea vikwazo vinavyolenga shughuli za kiutu katika tawala nyingi zilizowekewa vikwazo.
Naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Dmitry Polyansky, aliyeongoza mkutano huo amesema tawala nyingi zilizowekewa vikwazo zinaingiliana na mipango ya ujenzi wa nchi zao pamoja na maendeleo ya kiuchumi, akitolea mfano wa nchi kama Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan, na kuzitaja hatua zilizochukuliwa dhidi ya Guinea Bissau hazifai.