MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imewaona Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na wenzake watatu wana kesi ya kujibu katika mashtaka matano ya ugaidi yanayowakabili.
Mahakama imemwachia huru mshtakiwa wa kwanza Halfani Bwire kwa shtaka la sita baada ya kuona hana kesi ya kujibu. Shtaka hilo linahusu kukutwa na vifaa vya jeshi zikiwamo sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Uamuzi wa mahakama ulitolewa jana mbele ya Jaji Joachim Tiganga baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 13 wa upande wa mashtaka na vielelezo 39.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Tiganga alisema Mahakama ilipitia ushahidi ulioletwa na upande wa mashtaka kwa maneno na vielelezo ili kupima na kuona kama una chochote cha kuifanya iwatake washtakiwa kujitetea.
Jaji alisema katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Mei Mosi na Agosti 5, 2020 maeneo ya Hoteli ya Aishi, mkoani Kilimanjaro, washtakiwa walikula njama ya kutenda vitendo vya ugaidi, kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko ya watu kwa lengo la kusababisha hofu kwa Watanzania.
Kosa la pili inadaiwa washtakiwa wote wanne walikula njama za kutenda kosa la kumjeruhi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na lengo ilikuwa kuleta hofu kwa Watanzania.
Kosa la tatu kwa mshtakiwa wa nne Mbowe, anadaiwa katika mikoa ya Morogoro na Dar es Salaam alitoa fedha Sh 6,999 kwa washtakiwa wengine akijua zitatumika kwa ajili ya kuwapata wahusika kwa ajili ya kulipua vituo vya mafuta Mwanza, Dar es Salaam, Arusha lengo ikiwa ni kuleta madhara kwa Watanzania.
Shtaka la nne kwa washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa katika maeneo ya Aishi Hoteli mkoani Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, walishiriki kikao cha nia ya kupanga ugaidi na wanadaiwa walipanga kulipua vituo vya mafuta, mikusanyiko ya watu na vitendo hivyo vililenga kuleta hofu na madhara kwa raia.
Katika shitaka la tano, mshatakiwa wa pili, Adamu Kasekwa, anadaiwa Agosti 5, 2020 katika eneo la Rau Madukani, alikutwa na bastola aina ya Ruger A 5340 ikiwa na risasi tatu kwa lengo la kusaidia utendaji wa vitendo vya ugaidi kwa kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Arusha.
Shitaka la sita, Halfani Bwire, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, anadaiwa Agosti 10, 2020 eneo la Kilakala wilayani Temeke, alikutwa akimiliki vifaa kadhaa vya jeshi zikiwemo sare za JWTZ na JKT.
"Kwa kipindi chote cha kesi mawakili wa serikali walikuwa 8 huku utetezi kwa ujumla wakiwa 19. Jukumu la mahakama ni kupitia ushahidi ili kujua kama kuna kesi au la. Mahakama imepitia ushahidi wote wa maneno na vilelezo ili kujibu swali moja kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la.
"Katika hatua hii ya kuangalia washtakiwa wana kesi au la, mahakama inatakiwa iangalie ushahidi kwa ujumla wake na haitakiwi iangalie kupima mashahidi kwa uzito wake.
"Katika shauri hili mahakama imetumia muda wa siku mbili kwa ajili ya kupitia ushahidi wote kuanzia shahidi wa kwanza hadi wa 13 na vielelezo vyote 39 na vile vitano vya utetezi," alisema Jaji Tiganga.
Alisema katika uamuzi kwa shtaka la sita, linalomkabili Bwire la kukutwa na vifaa vya jeshi, ushahidi ulioletwa ambao ulikuwa ni vielelezo hivyo, mahakama ilikataa kwa sababu upande wa mashtaka ulikiuka maelekezo ya sheria ya ukamataji na hakuna ushahidi ambao umeletwa mahakamani kwa ajili ya mshtakiwa kujitetea.
"Kwa shtaka la sita, mshtakiwa Bwire hana kesi ya kujibu, hivyo inamwachia huru. Kwa shtaka la kwanza, pili, tatu, nne na tano, mahakama imefanya uchambuzi na imepitia vielelezo. Katika hatua hii, mahakama imeona upo ushahidi umeleta tuhuma dhidi ya washtakiwa, hivyo wana kesi ya kujibu katika mashtaka matano.
“Wanatakiwa walete utetezi, wanaweza kujitetea wenyewe au kuleta mashahidi na wanaweza kukaa kimya au wanaweza kutoa ushahidi wao kwa kiapo au bila kiapo,” alisema.
Baada ya kumaliza kusoma uamuzi, Jaji alitoa nafasi kwa upande wa utetezi kueleza utaratibu wa utetezi ndipo Wakili Jeremiah Mtobesya akadai kuwa wamepokea uamuzi na kwamba mshtakiwa wa kwanza ana kosa la kujibu katika shtaka la kwanza, pili na la nne, hivyo atajitetea mwenyewe chini ya kiapo na anatarajia kuita mashahidi wengine watano na yeye atakuwa wa sita na vielelezo vitano.
Wakili John Mallya kwa niaba ya mshtakiwa wa pili, Kasekwa ambaye amebaki na shtaka la kwanza, pili, nne na la tano ambalo anashtakiwa pekee yake, anatarajia kuleta mashahidi watatu na yeye atakuwa wa nne pamoja na vielelezo vinne.
Wakili wa mshtakiwa wa tatu, Ling'wenya, Fredrick Kihwelo, alidai mteja wake atajitetea kwa kiapo, atakuwa na mashahidi sita na vielelezo sita wakati Wakili Peter Kibatala akidai Mbowe atajitetea chini ya kiapo na atakuwa na mashahidi 10 na mwenyewe 11 pamoja na vielelezo 20.
Kutokana na uamuzi huo uliowakuta wana kesi ya kujibu, washtakiwa wataanza kujitetea Machi 4, mwaka huu.