MABOSI wa Simba wamemrejesha kikosini, Bernard Morrison, lakini wakimpa dakika 180 za mechi mbili zilizopo mbele yao ili kuona kama anapaswa kuendelea kubaki klabuni, licha ya kufahamu kila kitu juu ya kutakiwa na watani wao, Yanga.
Awali, alipewa mechi tatu, lakini juzi usiku aliingizwa kipindi cha pili katika mchezo wa Kombe la ASFC dhidi ya Ruvu Shooting na aliisaidia timu hiyo kupata mabao mawili wakati Wekundu wakiwasasambua maafande hao kwa mabao 7-0.
Winga huyo Mghana alitua Simba akitokea Yanga ambako alikuwa na vibweka vya aina yake alivyovihamishia hadi Simba mpaka kufikia kusimamishwa kutokana na utovu wa nidhamu kabla ya kurejeshwa tena kikosini siku chache zilizopita.
Nyota huyo alisimamishwa kutokana na makosa ya kujirudia rudia ya kutoroka kambini akidaiwa kuruka ukuta lakini ameomba msamaha kwa uongozi wake na kujumuishwa na wenzake juzi.
Habari kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo zinasema kuwa, baada ya kuomba radhi na kurejeshwa ametakiwa kuonyesha uwezo wake ambao wanauamini wao katika michezo mitatu mfululizo, ikiwamo mechi ya juzi ya ASFC dhidi ya Ruvu Shooting.
Mtoa habari huyo alisema, wanaamini na uwezo wake na ndio sababu iliyowafanya kumsajili lakini endapo atashindwa kuonyesha uwezo wanaoujua atakuwa amejipa mkono wa kwa heri yeye mwenyewe.
“Morrison ni mchezaji mzuri lakini anafanya makusudi kwa maslahi yake mwenyewe, sisi hatuna shida wala ugomvi naye, kaomba msamaha tumemuelewa na kumrejesha kundini,” kilisema chanzo chetu kilichoomba kuhifadhiwa jina na kuongeza;
“Kila kitu kinachoendelea tunakijua na hakuna siri ila kama anataka kwenda anakopajua yeye sio kuigharimu timu wakati kiwango chake tunakifahamu sisi.”
Chanzo hicho kilieleza, mechi hizo tatu ni zozote ambazo atapata nafasi ya kupangwa na kocha wao Pablo Franco.
“Ikitokea hizo mechi tatu akaonyesha kitu tunachomjua sisi tutamfikiria lakini akishindwa kuonyesha hivyo tutaachana naye aende anakotaka yeye hakuna shida, kwa kuwa hakuna mchezaji aliyeandikiwa Simba milele,” alisema mtoa habari huyo.