Maskini...Anayeidai TRA Sh986 milioni adai kutishiwa maisha



Mfanyabiashara Ramadhani Ntunzwe ‘Babu Rama’ akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Kwa takribani miaka sita sasa, mfanyabiashara Ramadhani Ntunzwe ‘Babu Rama’, ameendelea kupaza sauti kudai fidia ya Sh986 milioni kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku akidai kutishiwa maisha na watu wanaodaiwa kuwa maofisa wa mamlaka hiyo.

Mfanyabiashara huyo kwa mara ya kwanza aliwasilisha kilio chake Februari 28, 2019 katika kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wafanyabiashara wa Ilala ikiwa ni miezi saba tangu alipokutana na mkasa huo Oktoba 30, 2016 alipokuwa akisafirisha mzigo wake kutoka Afrika Kusini kupitia mpaka wa Tunduma kuelekea Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, Ntunzwe alieleza mikasa miwili iliyomkuta dhidi ya TRA; kwanza kushikilia mzigo wake kwa miaka mitatu kwa tuhuma za kukwepa kukodi huku yeye akidai kukataa kutoa rushwa ya Sh2milioni na mkasa wa pili ni kuibiwa mali zake zenye thamani ya Sh986 milioni katika duka lililopo Kariakoo baada ya TRA kulifunga kwa madai ya kutotumia mashine ya EFD.

Katika kikao hicho, Majaliwa aliagiza mfanyabiashara huyo arudishiwe mzigo wake baada ya kujiridhisha huku akiagiza ofisa wa TRA akamatwe. Miezi minne baadaye, Rais John Magufuli aliagiza TRA kuhakikisha wanalipa fidia zake, wakati huo Makamu wa Rais akiwa Samia Suluhu Hassan.


Wiki iliyopita Ntunzwe alijitokeza mbele ya wanahabari kumuomba Rais Samia kuingilia kati madai hayo, ili alipewe fidia yake hiyo inayotokana na hasara ya upotevu wa mali zilizoibiwa dukani kwake Kariakoo.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema majadiliano kati ya mfanyabiashara huyo na TRA yanaendelea ikiwamo masuala ya madai yake. “Hadi wiki hii mfanyabiashara huyo alikuwa anaendelea na mawasiliano na watalaamu wetu.

“Sasa changamoto ni kwamba Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015, kifungu cha 21 kinazuia kutoa taarifa za mlipa kodi, ni faragha kati ya TRA na yeye (Ramadhani Ntunzwe), kwa hiyo nisingependa kueleza kwa kina,” alisema Kayombo.


Kuhusu madai ya vitisho, Kayombo alimshauri kutoa taarifa kituo cha Polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamshna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhani Kingai alisema ofisi yake iko wazi kupokea malalamiko kuhusu changamoto za usalama wake.

“Tukipokea madai lazima tuchunguze, sasa sina uhakika kama amesharipoti kwa sababu vituo ni vingi, kama alishatoa taarifa inabidi atueleze kituo gani, ili tufuatilie taarifa zake,” alisema.

Alichokiomba

Alisema Agosti 9, 2020 alimuomba rais kwa wakati huo John Magufuli na alipokea kilio chake dhidi ya TRA, hivyo sasa anamuomba Rais Samia kumsaidia apate haki yake.


“Makubaliano ilikuwa Machi mwaka jana niwe nimelipwa haki zangu zote lakini mpaka sasa sijalipwa. Naimani mtanisaidia kufikisha taarifa hii kwa Rais Samia,” alisema.

Mkasa ulivyokuwa

Sakata la Ntunzwe lilianza Oktoba 2016 alipokuwa akisafirisha mzigo wake kutoka Zambia kupitia mpaka wa Tunduma.

Baada ya kufika Mbezi, Dar es Salaam, alikamatwa na maofisa wa Jeshi la Polisi akimtaka atoe ‘mzigo wa kufa mtu’ ili wamuache, lakini alikataa.

Mbele ya Majaliwa, Ntunzwe alisema ofisa wa TRA alipofika alitaka rushwa ya Sh2milioni, lakini alikataa.


Alisema suala hilo liliendelea kuwa kubwa baada ya maofisa hao wa TRA kumhusisha na makosa ya kukwepa kodi kabla ya kutaifisha mali zake. Novemba 22, 2017 TRA ilitoa kibali kwa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart kufungua duka hilo. Baada ya kufungua mali zote hazikuwemo ndani.

Alivyopambania haki

Desemba 2, 2020 alipata mwaliko wa kikao cha kutafuta suluhu ya madai yake ofisi za makao makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, mjini Dodoma kilichokuwa na wajumbe nane chini ya mwenyekiti aliyejitambulisha kuwa kaimu katibu mkuu wa wizara hiyo, Adolf Ndunguru.

Ajenda mbili za kikao hicho zilikuwa ni TRA kutoa ufafanuzi wa kutolipa madai ya mfanyabiashara hiyo licha ya Rais Magufuli kuagiza pamoja na ufafanuzi wa kufunga duka lake hatua iliyosababisha upotevu wa Sh986 milioni huku wakiwa wameshikilia mzigo wake kwa miaka mitatu mfululizo.

Kikao hicho kilikwama baada ya pande zote kutakiwa kuwasilisha nakala za hukumu. Kikao cha pili kilifanyika Februari 15, Dar es Salaam baada ya mvutano wa ukweli kuhusu kesi aliyodaiwa kuifungua Ntunzwe dhidi ya TRA katika Mahakama ya Wilaya iliyopo Kinyerezi, akidai fidia ya mali zake.

Katika kikao hicho cha pili, Ntunzwe aliwasilisha nakala ya hukumu akithibitisha katika kesi hiyo alikuwa mshtakiwa wa TRA wa makosa ya kutokutoa mashine ya EFD, kutokubandika TIN namba dukani kwake na kutokutoa ushirikiano. Kesi hiyo alidai kushinda.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad