Mastaa Simba watoa azimio zito, Chama aeleza



HAINA kufeli, ndiyo tamko walilotoka nalo Simba katika kikao cha wachezaji peke yao walichokaa chini ya manahodha wao kikilenga kubadili hali ya mambo na kutetea taji lao la Ligi Kuu Bara kwa mara ya tano mfululizo.

Kabla ya ushindi wa 6-0 dhidi ya timu ya Daraja la Pili ya Dar City katika mechi ya hatua ya 32-Bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Simba ilikuwa haijafunga bao hata moja katika mechi tatu zilizopita mfululizo za Ligi Kuu Bara ambazo waliambulia pointi moja na kupitwa pointi 10 dhidi ya vinara, Yanga.

Vipigo viwili na sare moja katika mechi tatu hizo za Ligi Kuu, vimewastua sio mashabiki peke yao bali pia wachezaji ambao wamekutana na kuamua kuanza upya ligi chini ya kauli mbiu kwamba kila mechi sasa ni fainali.

Kwenye kikao hicho kilichokaa kabla ya mechi ya juzi usiku, baadhi ya wachezaji waliongea ikiwemo manahodha, John Bocco na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kisha wakatoka na jibu moja kuwa kila mechi iliyokuwa mbele yao ni fainali.


 
Wachezaji walimueleza kocha wao kuwa huu si wakati tena wa kuangalia yaliyopita ila watayachukua kama fundisho katika mechi zijazo na hakuna mpinzani watakayemuacha salama kuanzia sasa.

“Ebwana eehh, wachezaji wa Simba sasa tumekubaliana hakuna kuangalia tunacheza na nani, wapi, bali kikubwa ni kama fainali na tunataka ushindi sasa kwani heshima yetu kama imeshuka na kuchukulia wa kawaida,” alisema mmoja wa wachezaji waandamizi kwenye kikosi hicho.

CHAMA AELEZA

Wakati hayo yakijiri, kiungo wa Simba, Clatous Chama amepiga stori na Mwanaspoti na kueleza yanayomzunguka tangu aliporejea Msimbazi katika dirisha dogo la usajili, wachezaji wa timu hiyo.


Chama ambaye anatazamwa na mashabiki wengi wa timu hiyo kama mtu sahihi anayekuja kuamsha morali iliyopungua klabuni, amesema ana muda mfupi tangu amejiunga na kikosi hicho ambacho kina mabadiliko kwahiyo si rahisi kuingia na kuanza kucheza katika kiwango cha juu moja kwa moja hadi apate muda zaidi.“Wakati nikiendelea na hilo huku mechi za ligi na mashindano mengine zinaendelea kwahiyo natakiwa kujituma zaidi ya vile ilivyokuwa mchezo uliopita na kuipa Simba mafanikio ya ushindi,” alisema Chama na kuongeza;

“Ukiangalia mechi mbili zilizopita ni tofauti kabisa na ambavyo nimetumika na Dar City kuna vitu vimeongezeka ikiwemo kuelewana vizuri na wenzangu na ninaamini baada ya muda mfupi kama mwezi mmoja tu itakuwa vizuri zaidi.

“Unajua wakati huu ligi ina ushindani mkubwa na kila timu inayokutana na Simba inatamani kupata matokeo mazuri kutokana na mafanikio tuliyokuwa nayo sasa hilo wachezaji tumelichukua kama changamoto na muda si mrefu mambo yatabadilika na kuwa mazuri.”

Alisema kikosi cha Simba kina uwezo wa kutetea mataji mawili Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (ASFC), kutokana na kiu ya mafanikio waliyonayo. Amewataka pia kubeza kejeli za washindani wao na kwamba sasa ni muda wa kuwa kitu kimoja.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad