KOCHA Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amefunguka kuwa benchi la ufundi la klabu hiyo halijaridhishwa na mwenendo wa ufungaji mabao ndani ya kikosi chao na tayari wamekaa na mastraika wa kikosi hicho kuangalia namna ya kumaliza tatizo hilo.
Simba msimu huu wamekuwa na changamoto kubwa kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambapo kabla ya mchezo wa jana walikuwa wamefanikiwa kufunga mabao 15 tu, katika michezo yao 14 ya mzunguko wa kwanza waliyokuwa wamecheza.
Kwenye Ligi Kuu Bara mpaka sasa kwa Simba ni Meddie Kagere pekee ambaye amefanikiwa kuandikisha mabao msimu huu akiwa tayari amefunga mabao matano, huku John Bocco na Chris Mugalu wao wakiendelea kuwa na ukame wa mabao.
Akizungumzia changamoto ya safu yao ya ushambuliaji msimu huu, kocha Matola alisema: “Kama benchi la ufundi tunakiri kuwa ni kweli tumekuwa na changamoto katika safu yetu ya ushambuliaji msimu huu, tatizo ambalo kama benchi la ufundi tunalifanyia kazi ili kuhakikisha linamalizika na tunafunga mabao.
“Tayari tumekaa na washambuliaji wetu na kuangalia wapi tunakosea ili kurekebisha, pia kuwaweka wazi kuwa hatuhitaji kuona hali hii inaendelea.”
JOEL THOMAS, Dar es Salaam