Matawi Simba yacharuka Mwenendo Mbovu wa Timu yao



KLABU ya Simba imetumia zaidi ya saa tatu kujadili mwenendo mbovu wa timu yao kwenye Ligi Kuu, kisha kuchimba mkwara mzito wakitaka mambo yabadilike ili kuweza kula sahani moja na watani wao, Yanga inayoongoza msimamo.

Simba imeachwa kwa pointi 10 na Yanga licha ya kila timu kucheza mechi 13, kwani watetezi hao wamekusanya pointi 25, wakati watani wao wana 35 na kuwapa presha mashabiki ndipo juzi Jumamosi matawi ya klabu hiyo wakaitisha mkutano.

Mkutano huo maalumu wa ndani uliwakutanisha viongozi wa matawi ya klabu hiyo na Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu na ulifanyika kwenye majengo ya Shule ya Sekondari Jamhuri, iliyopo eneo la Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Mwanaspoti lililotinga kwenye mkutano huo lilishuhudia viongozi hao wa matawi wakiandika majina yao katika orodha ya waliohudhuria kuanzia saa 2 asubuhi na mkutano kuanza saa 4:30 hadi saa 7:48 mchana, lakini gazeti hili lilizuiwa kuingia ndani kusikiliza kilichojadiliwa.


Licha ya kikao hicho kuwa ni cha siri kubwa lakini Mwanaspoti ilipenyezewa ajenda kubwa katika mkutano huo kuwa ni matokeo mabovu ya timu yao na mjumbe mmoja alidokeza kuwa, kukosa matokeo mazuri yanawaumiza mno.

“Kumekuwa na hisia za kuwepo kwa hujuma na tumemtaka mwenyekiti wetu, Mangungu akalifanyie kazi na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, ili kuweka mambo sawa, wakati sisi tunafanya yetu kuwashughulikia wahusika,” alisema mjumbe huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina.

“Haiwezekani timu inacheza, lakini haipati matokeo katika mechi tatu mfululizo, hii sio sawa na mbaya baadhi ya wachezaji hawaonyeshi kujituma uwanjani,” alisema mjumbe huyo aliyedai mashabiki kukosa raha kutokana na kero za Yanga.

“Yanga kuongoza tu pale kelele nyingi, lakini timu yao inacheza na inafunga, sasa tunaoumia ni sisi, tumemwambia mwenyekiti waliangalie hilo.”

Mangungu alipoulizwa na Mwanaspoti kuhusu mkutano huo wa matawi, alisema kikao hicho kiliwahusu wao tu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad