Kamati ya Bunge ya masuala ya UKIMWI imebaini ongezeko la matumizi ya vidonge vya kuzuia mimba kwa Wasichana hasa wenye umri kati ya miaka 10 - 24 ambapo licha ya kuwa na lengo la kuzuia mimba, matumizi ya vidonge hivi ambavyo vimekuwa vikiuzwa kwa bei ya chini imebainika yamechochea maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Kamati imeeleza kuwa baadhi ya Wasichana wamekuwa wakiogopa zaidi mimba kuliko maambukizi ya VVU na hivyo wamekuwa wakitumia vidonge vya P2 kama njia mbadala ya kuzuia mimba na kuacha kutumia condom ambazo zingewakinga dhidi ya maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono na hata hizo mimba zisizotarajiwa.
Ili kukabiliana na tabia hii Kamati imeshauri kwamba wakati wa kuuzwa kwa dawa hizi za kuzuia mimba (P2) ni vizuri zikauzwa pamoja na condom kwa lazima ili kuwawezesha Wasichana kuwa na tabia ya kutumia condom hizo bila ya kunyanyapaliwa kwani uzoefu unaonesha kwamba iwapo watakuwa na hizo kondomu basi Wasichana wengi watazitumia ili kupunguza maudhi na madhara ya dawa za kuzuia mimba.