Mchungaji Lucy Nyawira Thuo kutoka nchini Kenya , amewashangaza wengi kwa ukakamavu wake wa kuzungumzia hali yake ya HIV hadharani na hata makanisani.
Hii ni hali ambayo mama huyu anaiona kama sehemu ya wito wake wa maisha kwamba atoe nasaha na awe kielelezo cha kuishi na virusi vya HIV kwa miaka mingi na kwamba ni kitu ambacho kinawezekana .
"Ni miaka miwili sasa tangu nilipoanza kuzungumza hadharani kuhusu hali yangu , mimi kama mwanamke anayekuwa kwenye maombi kila wakati nilifahamu kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa ananiita kwa watu ambao wanaishi na HIV , na huenda hawaoni mwanga wa maisha tena , Sasa mimi ninakuwa mwandani wa karibu wa makundi Haya ya watu hasa maeneo ninayoishi na sehemu ninayofanya ibada ." Anasema Lucy.
Mchungaji Lucy Thuo ni mama wa umri wa makamo , amekuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka ishirini na moja pia ni mama wa watoto wawili na bibi wa mjukuu mmoja . Ila pia simulizi ya kuambukizwa HIV na hatimaye mume wake kuifahamu siri hilo ni jambo ambalo mama huyu hatolisahau katika maisha yake .
Lucy alizaliwa Kaunti ya Nakuru , na anaelezea maisha ya mahangaiko yaliokabili jamii yao, alipewa malezi ya kwanza na mama kama mlezi wa kipekee , ila mama yake Lucy aliugua na kufariki angali binti , Lucy anasema kwamba wakati huo alielezwa kwamba mama alifariki kutokana na vidonda vya tumbo, japo baadaye alielezwa kwamba mama alifariki kutokana na ugonjwa wa ukimwi.
Baada ya kifo cha mama , Lucy hakumaliza shule aliamua kuhamia mji Mkuu Nairobi ambapo anakiri kwamba akiwa na umri wa miaka 17 alianza maisha ya ndoa na mwanaume wa miaka 30 , ndoa ambayo haikushika kasi na iliisha baada ya mwaka mmoja pekee .
"Nilikuwa natamani sana ndoa , nilikuwa naona kwamba kwetu na upande wa mama wanawake hawakuwa wanaolewa ila mimi nilijifariji kwamba lazima ndoa yangu ifaulu"Lucy anakumbuka.
Na Kwa hiyo Lucy alijaribu ndoa baada ya nyengine karibia mara nne hata moja isifaulu ila alishika mimba na kujifungua mwanaye ambaye alianza kuona malezi kama mzazi wa kipekee pia , majukumu ya kumlea mwanae na dada yake mdogo alimwachia bibi , huku Lucy akipambana na maisha mjini . Lucy anasema kwamba alikuwa mhudumu wa bar . Katika pula pilka hizo anakiri kujihusisha na mahusiano ya muda mfupi hapa na pale
"Unafahamu kwamba zamani kuwa mhudumu wa bar wa kike kulikuwa na changamoto mno , kwanza mshahara ulikuwa chini ya dola ishirini , wakati mwingi hata sikupokea mshahara huo hasa kama nilivunja bilauri au mteja kupotea bila malipo .
Tungekatwa pesa zetu kwa hasara hiyo . Kwa hiyo ilibidi niwe na mahusiano ya kimapenzi na wanaume tofauti ili kupata riziki japo sio kitu nilichokipenda " Lucy anasema.
Mwanadada huyu anakiri kwamba wakati mmoja alikuwa na marafiki wa kiume kama watatu kwa wakati mmoja , kila wakati akitafuta mwenye hela zaidi . Baada ya muda Lucy alikumbana na mtu ambaye angekuwa mume wake hadi leo , aidha mwanadada huyu anasema kwamba mwanzoni mwa mahusiano Yao ulikuwa tuu rafiki , ni urafiki uliokuwa kwa kasi mno na baada ya miezi saba Waliamua kuishi kama mume na mke .
Kukutwa na Virusi vya Ukimwi
Mwaka wa 2002 alishika mimba , na kama Ada ya hospitali ilimbidi afanyiwe vipimo katika kliniki ikiwemo ya HIV , katika shughuli hio Lucy alielezwa kwamba alikuwa mama mjauzito mwenye HIV , Lucy alishtuliwa mno na taarifa hio na alipofika nyumbani hakumweleza mume wake kuhusu hali yake .
"Nilipofika nyumbani Nilikuwa na uoga wa kufa, niliwazia mtoto aliyekuwa Tumboni na hata maisha ya mume wangu , ila si kuwa tayari kupasua mbarika kuhusu hali yangu , nilijieleza kimoyomoyo kwamba ikiwa mume wangu atafahanu kuhusu hali yake ya HIV sio kutoka kwangu " Lucy anasema
Lucy anasema kwamba mume wake alikuwa na mashaka baada ya yeye kutoka kliniki wakati alipopewa matokeo ya hali yake ya HIV , kwani aliporejea nyumbani na kwa siku kadhaa zilizofwata alikuwa Ana sikiliza nyimbo za mazishi, mama huyu anasema alikuwa anahisi kifo tu
Mtoto alipozaliwa , Hospitalini Lucy alikuwa alielezwa asimyonyeshe mtoto lakini kwa hofu ya mumewe asiju, yeye hakusikiliza madaktari, na aliendelea kumyonyesha mwanaye .
Ila miaka 7 baadaye mwanaye aliugua vibaya na ikabidi wote waende hospitali wote kwa ajili ya vipimo.
Ilikuwa mwaka wa 2008 walifanyiwa vipimo vya HIV , yeye mumewe na Mwana Wao. Kati ya hao ni Lucy pekee aliyepatikana na HIV . Ilikuwa ni siku ya aina yake , upande mmoja Lucy alikuwa na afueni kwamba hajawaambukiza mtoto na baba , upande mwengine alikuwa na maswali mengi kuhusu hatma ya ndoa yake na mume wake Kwani alikuwa hana virusi vya HIV.
"Kitu cha ajabu kilifanyika mume wangu hakuzungumzia swali hilo tuliporudi nyumbani , hakuniuliza ni vipi nina HIV , alikuwa mnyamavu mno katika swala hilo . Maisha yalisonga mbele huku mimi nikimeza madawa ya kupunguza makali ya HIV , kila siku ."Lucy anakumbuka
Mwanadada huyu anasema kwamba baada kufunga ndoa na mumewe yeye alianza maisha ya Kumcha Mungu kibinafsi , kwa lengo la kuelewa maisha yake yalikuwa yanaelekea wapi na pia kufuata masomo ya kidini kwa lengo la kuwa mchungaji, amekuwa akiongoza mikutano na nasaha kwa wenye kuishi na HIV , Mwanamke huyu anasema kuwa ni nadra kuwapata viongozi wa kidini wakijitokeza kuzungumzia hali Yao ya HIV ila yeye anasema imesaidia kuwapa matumaini hasa wanawake walioko maeneo ya kidini , na ni waathiriwa wa HIV .
"Njia inayofahamika ya kuambukizwa HIV ni mmoja , na mimi nakumbuka nyakati nilikuwa nahaha huku nakule nilikuwa mwangalifu mno , Kwa hiyo siwezi kujua ni nani aliyeniambukiza mpaka leo " anakumbuka Lucy.
Lucy amekataa dhana iliyokuwepo katika jamii yake kwamba huenda kulikuwa na laana kwa kuwa Mama yake mzazi , shangazi wale wawili na mjomba mmoja walifariki na HIV , na huenda ilimwandama pia , ila yeye mwenyewe anamini kuwa wakati huo tabia yake haikuwa Sawa na tayari amerekebisha hilo .
"Mimi nimebadilika na kuwa kiumbe kipya kabisa , yakale yamepita na hivi Sasa ninaishi kwa kuzingatia nidhamu katika maisha yangu " anasema Lucy