Meli kubwa kuanza kutia nanga Bandari ya Tanga mwezi ujao
BANDARI ya Tanga maarufu kama ‘Lango la Kaskazini’ itaanza kuingia katika ushindani na bandari nyingine, baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya miradi miwili inayotekelezwa kwa zaidi ya Sh bilioni 468 na kuwezesha meli kubwa kutia nanga.
Miradi hiyo miwili ya uboreshaji wa bandari hiyo, mmoja umeshafikia asilimia 95 na mwingine ukamilishaji ukiwa katika asilimia 25.
Kukamilika kwa miradi hiyo miwili kutawezesha meli kubwa kutia nanga katika gati na kupakua mizigo au kushusha abiria, huku ikiwa haina shaka na kina cha bahari ambacho kwa sasa kimeongezwa kutoka mita tatu hadi 13.
“Kutokana na maboresho hayo, sasa tutaweza kuhudumia mizigo ya zaidi ya tani milioni mbili kutoka kiwango cha sasa cha tani 730,000 kwa mwaka," alisema Mkuu wa Idara ya Utekelezaji, Colman Moshi.
Alisema kukamilika kwa mradi huo sasa meli zinapakua mizigo mita 200 kutoka eneo linalojengwa gati na ifikapo Machi gati itaanza kutumika rasmi kwani kazi ya uchimbaji kuongeza kina kufikia mita 13 itakuwa imekamilika na kuwezesha meli kubwa kutia nanga.
Awali, meli zilikuwa zinapakua mizigo kilomita 1.7 kutoka eneo la gati na hivyo kusababisha gharama kuwa kubwa na kutumia muda mrefu kushusha shehena.
“Tumejiweka katika ushindani na bandari jirani. Kina kinaongezwa kuwezesha meli kufika bandarini na mitambo mipya na yenye uwezo mkubwa imeletwa kuongeza uwezo wa bandari. Kwa sasa hali tuliyonayo tupo katika nafasi nzuri zaidi ya kutumia fursa ya ukaribu na wateja wetu kuongeza Pato la Taifa,” alisema.
Moshi alisema Bandari ya Tanga sasa ni shindani kutokana na kuwa jirani na mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia.
Aidha, alisema kutokana na marekebisho ya tozo na kuimarishwa kwa usalama wa shehena, bandari hiyo inabebwa na miundombinu ya barabara na reli iliyokamilika na inayoendelea kujengwa kuelekea maeneo ya kati ya Tanzania, Kaskazini na Kanda ya Ziwa.
Moshi alisema kutokana na kuboreshwa kwa bandari malengo yao yamebadilika na kwamba mradi mzima ukikamilika itaweza kuhudumia shehena ya tani milioni tatu.
Ofisa mipango na takwimu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari TPA, Bandari ya Tanga, Joseph Mwambipile alisema kwamba mwaka huu wa fedha kwa maboresho yanayoendelea wamepanga kuhudumia mizigo na meli zaidi ya 129 na hadi Desemba mwaka jana wamehudumia meli 88.
Alisema bandari hiyo yenye uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena za mizigo mbalimbali, mafuta na abiria, imelenga kuhudumia makasha 20,000 na abiria 99,000 mara tu mradi kamili utakapokamilika Oktoba, mwaka huu.