MFUNGWA mmoja aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 gerezani na mahabusu aliyekuwa na tuhuma za mauaji, wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Magereza wakati wakijaribu kutoroka kwenye Gereza Kuu la Lilungu mkoani Mtwara.
Mauaji hayo yanadaiwa kutokea Desemba 17 mwaka jana majira ya saa sita mchana yakimhusisha mfungwa mwenye namba 321/2021 Juma Mohamed Mwanya na mahabusu mwenye namba ya kesi PI. 2/2020 Dionis Robat, aliyekuwa ameshtakiwa kwa kosa la mauaji katika Mahakama ya Wilaya ya Lindi.
Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi Raymond Mwampashe, aliiambia Nipashe jana kuwa mauaji hayo yalifanyika nje ya gereza baada ya mmoja wa waliotoroka kumshambulia kwa kitu kizito usoni askari mwenye namba B.S. 5427 Bamila Maneno.
Alidai mauaji hayo yalitokea majira ya saa sita mchana Desemba 17 mwaka jana baada ya jitihada mbalimbali za askari magereza kuwataka wahusika wajisalimishe kushindikana.
"Kwa taarifa nilizoletewa, hawa waliouawa walifanikiwa kuruka ukuta wa ngome ya magereza muda huo wa mchana na askari wetu waliposhtuka wakapiga filimbi kwa ajili ya kuwazingira lakini walishatoka nje ya gereza na kukimbilia kwenye mashamba ya korosho, hivyo jitihada za kuwatafuta zilianza mara moja kwa askari kuzunguka kila eneo huku wawili wakienda na pikipiki kuzuia barabara kuu," alidai.
Aliongeza kuwa wakati msako ukiendelea askari magereza waliokuwa na pikipiki walikutana na askari wa usalama barabarani na walipowauliza kama wamewaona wafungwa wakipita katika eneo hilo, wakawaambia wameona watu wawili wamepita wakiwa wanakimbia baada ya kuvuka barabara ya kuelekea Newala.
Alidai kuwa baada ya taarifa hiyo, askari walizunguka msitu uliokuwa karibu na eneo waliloelekezwa na wakati msako ukiendelea mwenzao mmoja alipigwa na kitu kizito na mmoja wa waliotoroka huku wakimfuata askari mwenye silaha ili kumpokonya.
Mwampashe aliongeza kuwa hata walipoambiwa wajisalimishe walikataa na wakawa wanazidi kuwakabili askari ndipo walipopigwa risasi kisha wakachukuliwa kwa ajili ya kuwahishwa Hospitali ya Ligula baada ya taratibu za kipolisi katika eneo hilo kukamilika, lakini walifariki dunia baada ya kuvuja damu nyingi.
Alipoulizwa maeneo ya mwili waliyopigwa risasi, Mwampashe alidai hilo ni suala la kipolisi kwa kuwa wakati tukio linatokea hakuwapo mkoani Mtwara.
Akizungumzia tuhuma zilizowafikisha gerezani mfungwa na mahabusu waliouawa, Mwampashe alisema mahabusu alikuwa na kesi ya tuhuma za mauaji katika Wilaya ya Lindi na alihamishiwa Gereza Kuu la Lilungu Oktoba 9 mwaka jana akiwa anatumikia kifungo cha miaka miwili baada ya kujaribu kutoroka wakati akisubiri kesi yake ya mauaji iendelee huko Lindi.
“Huyu mahabusu Robart alishajaribu kutoroka katika Gereza la Nachingwea wakati akisubiri kutajwa kwa kesi yake, na alipokamatwa ndiyo akahukumiwa miaka miwili kwa kosa la kutoroka ndani ya gereza, kifungo chake kwa kosa hilo alimaliza Desemba 11 mwaka jana," alidai.
Mwampashe aliendelea kudai kuwa mfungwa Mwanya aliyejaribu kutoroka alikuwa kwenye kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kuhukumiwa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Ruangwa Julai 26 mwaka jana kutumikia adhabu hiyo alipokutwa na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
“Huyu Mfungwa mwili wake tuliwakabidhi ndugu zake lakini mahabusu alizikwa na manispaa baada ya jitihada za kutafuta ndugu zake huko mikoa ya kanda ya ziwa kushindikana," alidai.
Mauaji hayo yametajwa kipindi ambacho serikali imeunda tume ya kuchunguza mauaji ya mfanyabiashara yanayodaiwa kufanya na baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara mwanzoni mwa mwaka huu.