Dodoma. Mgombea nafasi ya Spika wa Bunge kupitia Chama cha AAFP, Ndonge Said Ndonge amelitumia Bunge kuvuna fedha wakati akijinadi kuomba kura kwa wabunge.
Ndonge amewagusa wabunge kwa kauli yake kuhusu kazi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan hasa kwenye ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2022.
Uchaguzi wa Spika unafanyika leo kufuatia kujihuzulu kwa aliyekuwa Spika, Job Ndugai Januari 6, 2022 na jumla ya watu 9 wamejitokeza kugombea nafasi hiyo.
Katika maelezo yake kwa wapiga kura, mgombea huyo alisifia mambo mengi ya Serikali lakini akasema uwezo wa kuyafanya mazuri zaidi anao akiwa Spika na akaomba wagombea wenzake wajitoe kwenye kinyang'anyiro.
Amesema "Mama ameupiga mwingi hadi Kawe madarasa yamejengwa, zamani kulikuwa na uchaguzi hadi mara nne kwa wanafunzi kuchaguliwa kidato cha kwanza hadi wengine walikuwa wameshaozwa ndio simu zinapigwa kuwa binti kafaulu,"
Wakati akijieleza, alisimama Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na kumfuata kwenye mimbari akampa fedha.
Hata hivyo alipomaliza kujieleza, wabunge walimiminika kumfuata na kumpa fedha nyingi zikionekana ni noti za Sh10, 000 ambazo idadi yake haikujulikana.
Mwenyekiti wa uchaguzi huo, William Lukuvi amewaambia wabunge kuwa sio dhambi wala si rushwa kwani wapiga kura ndiyo wanaotoa si mgombea hivyo akasema wenye kumpa wampe na hata akiwa ametoka wanaweza kumpelekea.
Ndonge ni mgombea mwenye ulemavu wa ngozi ambaye amesimama mbele ya Bunge kwa kujiamini na kujieleza kwa ufasaha zaidi.