Mikopo ya vikundi inavyopigwa Bungeni



Mbunge wa Ulyankulu, Rehema Migila akichangia bungeni kuhusu jinsi mikopo ya vikundi katika halmashauri inavyotumika vibaya, juzi. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Ni kilio cha ubadirifu wa fedha za mikopo inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika maeneo mengi ya nchi.

Wakati wabunge wakipigia kelele ubadhirifu wa fedha hizo zilizokusudiwa zirejeshwe ili zisaidie watu wengine, wadau wameshauri sekta binafsi ihusishwe katika kamati za mikopo na utoaji elimu ya biashara ili kuondokana na tatizo hilo.

Juzi Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), David Silinde alikiri kuwepo kwa ubadhirifu katika mikopo hiyo, akasema wanakusudia kubadili sheria na kanuni za mikopo hiyo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

“Tunakwenda kuleta marekebisho ya sheria na kanuni za jinsi ya utoaji wa fedha hizo kwenye halmashauri zetu nchini, kilio cha wabunge tumekisikia na hata sisi tumeliona hilo kwani inawezekana mfumo wake siyo rafiki,” alisema Silinde.


Kauli ya Silinde imekuja, huku kukiwa na taarifa za Takukuru Wilaya ya Temeke kuchunguza kiongozi mmoja wa CCM kwa madai ya ubadhirifu wa Sh300 milioni za mikopo hiyo.

Hata hivyo, kiongozi huyo alipozungumza na Mwananchi hivi karibuni alisema tuhuma hizo hazina ukweli wowote na kwamba huo ni mkakati wa kutaka kumchafua kuelekea kwenye changuzi wa ndani ya chama.

Akizungumza wakati akipokea ripoti ya uchunguzi wa mikopo hiyo mbele ya viongozi wa wilaya hiyo hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo aliiagiza Takukuru na Polisi kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua haraka.


Suala la kutorejeshwa kwa fedha za mikopo hiyo limekuwa sugu na limekuwa likibainishwa katika ripoti ya Mkadhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) katika halmashauri nyingi kila mwaka.

Julai mwaka vikundi vya wanawake wa CCM katika Wilaya ya Kinondoni waliwatuhumu hadharani maofisa maendeleo ya jamii kwa kuunda vikundi hewa na kujinufaidha ana mikipo hiyo.

Kelele za wabunge

Wakijadili jana bungeni jijini Dodoma, wabunge takriban saba walilalamikia ubadhirifu wa fedha hizo na kuitaka Serikali isistishe mikopo hiyo, kwa kuwa imetengeneza mianya ya rushwa na ufisadi kwenye halmashauri.

Walisema fedha hizo zimeshindwa kuwa mkombozi wa kuinua pato la maisha kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.


Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Abdallah Chaurembo alisema halmashauri za wilaya na miji zilikuwa zimetoa zaidi ya Sh70 bilioni kwa makundi hayo lakini hakuna tija iliyoonekana ndani yake.

Chaurembo alisema maeneo mengi kamati ilipokwenda kuhoji ilionekana hawana taarifa sahihi bali wanachokijua ni kiasi walichotoa lakini nani alichukua, yuko wapi au anafanya nini hawakuwa na taarifa.

Miongoni mwa wabunge waliozungumzia suala hilo ni Rehema Migila wa Ulyankulu aliyesema Serikali inachokifanya ni kuchoma pesa barabarani kwa kuwa hakuna faida yoyote katika asilimia 10 za halmashauri na kwamba zimeshindwa kubadilisha maisha ya wanyonge.

Migila alisema alisema iwe iwavyo fedha hizo hazitaweza kubadilisha maisha ya wanyonge wala kupeleka kwenye malengo makubwa ambayo Serikali ilikusudia.


Kwa upande wake Mbunge wa wa Hai, Saashisha Mafuwe alisema fedha hizo zinaliwa mno na watendaji katika maeneo mengi ya halmashauri na hutolewa kwa ubaguzi.

Mafuwe alitolea mfano wa ubaguzi kwamba zinatolewa kwa vijana wasiozidi umri wa miaka 35, wakati kundi kubwa la umri huo ndiyo wanamaliza masomo na kuanza maisha lakini wenye uzoefu wa biashara lakini wametengwa.

Akisisitiza kuhusu ubadhirifu huo, Jakline Msongozi alitaja mfano wa wilaya ambazo fedha zimetumika vibaya kuwa ni Temeke ambako alisema kuna diwani mmoja alitengeneza vikundi vingi hewa halafu akakusanya fedha hizo na kuingiza kwenye miradi yake biafsi.

Tatizo linajirudia

Kwa mujibu wa ripoti za CAG suala la ubadhirifu wa fedha hizo si jipya na katika mwaka ulioishia Juni 30, 2020 katika halmashauri 130 mkaguzi huyo alibaini kuwa mikopo ya Sh27.79 bilioni ilikuwa haijarejeshwa.

“Hii inaonyesha kwamba halmashauri husika hazikufuatilia kwa ukaribu marejesho ya mikopo kutoka kwa vikundi kulingana na makubaliano, ilisema ripoti hiyo.


Ajabu ni kwamba CAG alibainisha kuwa kiwango cha mikopo isiyorejeshwa kwa miaka minne mfululizo imekuwa ikiongezeka kila mwaka, hali aliyosema “inamaanisha kuwa halmashauri hazikufanya jitihada katika ukusanyaji wa mikopo.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa mwaka 2016/17 katika halmashauri 84 mikopo ya Sh5.8 bilioni haikurejeshwa wakati mwaka uliofuata, 2017/18, katika halmashauri 90 fedha za mikopo zilizotafunwa nu Sh10 bilioni.

Katika 2018/19 wakopaji kwenye halmashauri 111 walitokomea na Sh13.79 bilioni na kwa mwaka 2019/20 fedha zilizopotea ni Sh27.79 bilioni katika halmashauri 130.

Kufuatia hali hiyo CAG alipendekeza menejimenti za Mamlaka za Serikali za Mitaa zifanye ufuatiliaji wa karibu ili mikopo hiyo iwe inarejeshwa kwa mujibu wa makubaliano na pia, kufanyike uhamasishaji na kujenga uelewa wa ulazima na umuhimu wa kurudisha mikopo bila shinikizo kwa lengo la kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Waliokithiri

Mbali na Temeke, changamoto za mikopo hiyo zilielezwa katika Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam Januari 2021 wakati aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Kisare Makori alipokabidhi zaidi ya Sh1 bilioni kwa vikundi 111 vya ujasiriamali, huku manispaa hiyo ikiwa inadai Sh1.7 bilioni zilizotolewa mwaka 2020.

Makori alisema mwaka wa fedha 2019 manispaa hiyo ilitoa Sh3.9 bilioni kwa vikundi 914 vyenye watu zaidi ya 9,281 lakini fedha zilizorejeshwa Sh1.3 bilioni tu.

Wakati Ubungo ikiendelea kutafuta fedha hizo, halmashauri ya Wilaya Chalinze mkoani Pwani imeshindwa kutoa mikopo ya mwaka 2020/21 kutokana na mzigo wa madeni ya mikopo iliyopita.

Wakopaji hawana sifa

Hali ikiwa hivyo, imeelezwa kuwa moja ya sababu za ubadhirifu wa mikopo hiyo ni pamoja na wakopeshwaji wengi kutokuwa na sifa na kukosa uvumilivu wa kutunza miradi wanayoiandikia.

Hayo yamebainika katika utafiti uliofanywa na Jukwaa Huru la Kilimo (Ansaf) Januari mwaka huu.

“Vijana hasa wa kiume hawana moyo wala uvumilivu wa kutumia fursa za kiuchumi zilizopo. Wanataka biashara za kupata faida za harakaharaka kama bodaboda, Bajaj, uchakataji, biashara za mikononi badala za shughuli za uzalishaji kama kilimo,” imesema sehemu ya utafiti huo.

Changamoto nyingine iliyotajwa ni ukosefu wa elimu ya utunzaji wa fedha na kuwa Mamlaka za Serikali za mitaa zinazotoa mikopo hazitoi elimu ya kutosha za kutunza fedha hizo wala elimu ya biashara, hivyo kushindwa kurejeshwa kwa fedha zilizokopwa.

Ripoti hiyo imeishauri Serikali na wadau kutoa elimu ya ujuzi kuhusu usimamizi wa biashara kwa wanufaika wa mikopo.

“Mikopo hiyo inapaswa kutolewa kwa walengwa wenye vigezo vya kueleweka wakiwa na maombi yenye maudhui ya kueleweka na waombaji watakaojitoa kuwajibika kwa mkopo waliyoomba,” imesema sehemu ya ripoti.

Mapendekezo mengine ni pamoja na kuihusisha sekta binafsi katika kamati za mikopo na wajumbe wenye ujuzi na maadili ili kuepusha hasara za kutorejeshwa kwa mikopo hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad