Dar ea Salaam. Wasimamizi wa mirathi ya aliyekuwa mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi, wameburuzwa mahakamani wakidaiwa kukataa kuwahudumia watoto wadogo wa mfanyabiashara huyo aliowazaa na mkewe Jacquiline Ntuyabaliwe.
Kesi hiyo imefunguliwa na Jacquiline katika Mahakama ya Watoto iliyoko katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.
Wasimamizi wa mirathi hiyo wanaokabiliwa na kesi ni mtoto wa marehemu, Abdiel Mengi na mdogo wa marehemu, Benjamini Mengi.
Habari ambazo Mwananchi limezipata na kuthibitishwa na wakili wa mjane huyo, Audax Kahendaguza, kwa ridhaa ya mteja wake, katika shauri hilo la madai namba 50 la mwaka 2022, Jacquiline anadai matunzo ya watoto hao ikiwamo ada ya shule.
Anadai kuwa watoto hao walikuwa wakigharimiwa ada na baba yao pamoja huduma nyingine zote walizostahili, kutokana na kipato alichokuwa anakipata kwenye shughuli zake za kibiashara, ambazo kwa sasa ziko mikononi mwa wasimamizi hao wa mirathi.
Anadai kuwa hata baada ya kifo cha baba yao, awali wasimamizi hao walikuwa wakiwalipia ada na huduma nyingine japo mara mojamoja; kwamba sasa wameacha kabisa kuwalipia ada ya shule pamoja na huduma nyingine licha ya kuwaomba mara kadhaa.
Mawakili wa wadaiwa walieleza kuwa hawajaandaa majibu ya madai hayo kwa kuwa wateja wao wako mikoani huku Mahakama ikiwataka kuwasilisha majibu yao Februari 17, mwaka huu siku ambayo pia kesi hiyo itatajwa tena.
Kesi hii imekuja wakati bado kuna mgogoro wa mirathi ya marehemu Mengi kati ya pande hizo mbili, kwani bado kuna shauri la mirathi linasubiri uamuzi.