Mkataba wa Morrison Yanga kufuru, Simba waitana



Mkataba wa Morrison ndani ya Simba umesaliwa muda usiozidi miezi mitatu na mabosi wa klabu hiyo wamemsimamisha kwa kudaiwa kutoroka kambini kwa kuruka ukuta, pamoja na kufanya vituko vingine kambini.
Lakini, habari za uhakika zinasema Mghana huyo aliyeondoka kwa kuwakera wanayanga anarejea tena kunako klabu hiyo iliyomleta nchini, baada ya matajiri wa klabu hiyo kumwekea mzigo wa maana ili kunasa saini yake.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, vigogo wawili wakubwa wa klabu hiyo wameungana kuanzisha vita ya kumbeba Morrison kwa kumwekea mezani dau zito na tayari jamaa amewajibu;”sina tatizo kurejea Yanga.” Mwanaspoti linajua kwamba Simba wamenasa mchongo huo na wikiendi hii walikutana Jijini Dar es Salaam kujadili ishu hiyo pamoja na mwenendo wa klabu yao.
Morrison katika mkataba wake na Simba umebakiza siku 90 tu kumalizika huku hatua ya mazungumzo ya mkataba mpya yakikwama muda mrefu, na sasa hatua mbaya ni kwamba ana kesi ya utovu wa nidhamu na Wekundu hao.
Itakumbukwa akiwa na Yanga, Morrison aliondoka kwa utata mkubwa kisha kesi yake kufika mpaka Mahakama ya michezo (CAS) na mchezaji huyo kuwabwaga mabosi wa Yanga.
Matajiri hao wawili ambao Mwanaspoti ina majina yao wamekubaliana kwamba wapambane kumchukua wakitaka ufundi wake bila kujali vurugu zake.
Habari ambazo Mwanaspoti inazifahamu na kuwa na uhakika nazo kwa asilimia 100 ni kwamba Morrison ameahidiwa ofa nzito ya dola 100,000 (Sh230 Milioni) kama ada ya usajili tu ambapo matajiri hao kila mmoja akichanga dola 50,000 (Sh 115 milioni).
Ofa hiyo imeushtua upande wa mchezaji huyo ambapo tayari wameshajibu kwamba wamekubaliana na wanasubiri kuona kipi Simba wataamua katika mashtaka yao. Mbali na dau hilo mshahara wake ameahidiwa atachukua dola 8,000 (Sh18.4 Milioni) sawa na kiasi ambacho analipwa kiungo wa Simba Clatous Chama sasa aliporejea Msimbazi.
Hata hivyo, umetokea mgawanyiko kwa baadhi ya mabosi wa Yanga kuhofia kiungo huyo anaweza kuwavuruga tena wakipendekeza hata akirudishwa asipewe mkataba mwepesi ili umfunge na kumtuliza. Huku wengine wakitaka atolewe kwa mkopo arejee Yanga kama ikifika hatua ya makundi ya Afrika msimu ujao.
“Tunamtaka Morrison kweli na kuna watu tumeshawapa kazi hiyo na inakwenda vizuri,ukiachana na tabia zake hakuna klabu ambayo itakataa kuwa na mchezaji mwenye kipaji kama kile,” alisema tajiri huyo ambaye hakutaka jina lake liwe gazetini.
“Hebu fikiria msimu ujao unakuwa na Mayele (Fiston) pale juu kulia una Moloko (Jesus) huku kushoto una Morrison na chini ya Mayele una Feisal (Salum) utakuwa na timu ya aina gani?Kuna wenzetu wanataka apewe mkataba mgumu kidogo wengine wanaogopa lakini tutakubaliana tu.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad