SHAHIDI wa 13 wa upande wa Jamhuri, Inspekta Tumaini Swila, amedai kuwa wakati anafungua jalada la kula njama kufanya uhalifu, mlalamikaji alikuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna wa Polisi Robert Boaz na mlalamikiwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.
Inspekta Swila alidai hayo jana Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Joackim Tiganga wakati akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali, Robert Kidando.
Akitoa ushahidi, alidai ni mkaguzi wa polisi, yuko Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Temeke na anafanya kazi ya upelelezi kwa miaka 24 sasa.
Alidai alikuwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) Julai 14 mwaka 2020, alimkuta DCI, Kamishna Boaz na Kamishna Msaidiz wa Polisi, Ramadhan Kingai.
Shahidi alidai kupokea maelekezo kutoka kwa Afande Kingai kuwa anatakiwa kufungua jalada la uchunguzi, DCI alipokea taarifa kutoka kwa Luteni Urio juu ya uwapo wa kundi linaloratibiwa na Mbowe kufanya uhalifu.
Alidai kundi hilo linaratibiwa kulipua vituo vya mafuta, kuchoma moto masoko, kukata miti kwenye barabara kuu ili kuzuia magari, kuwadhuru viongozi mbalimbali wa serikali kwa lengo la kuleta taharuki.
"Afande Kingai alitaka nifungue jalada la uchunguzi nilifungua, wakati ninafungua mlalamikaji alikuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna Robert Boaz na mlalamikiwa Freeman Mbowe.
"Nilifungua jalada la kutaka kufanya vitendo vya uhalifu, Kingai aliniambia nilihifadhi atanipa maelekezo, Julai 15 mwaka 2020, Kamishna Boaz alitaka nimsaidie Afande Kingai kufanya upelelezi," alidai shahidi huyo.
Alidai Kingai alimfahamisha kwamba Luteni Urio alishawapata vijana wa kuwapeleka kwa Mbowe na alimtaka afungue jalada la kesi Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.
Shahidi alidai alifungua jalada la kula njama kati ya Mei na Julai mwaka 2020 na kwamba kuna kundi la watu wanapanga kufanya vitendo vya kigaidi katika mikoa mbalimbali nchini.
"Afande Kingai alitaka nisiandike jina la mtuhumiwa Mbowe katika taarifa hiyo ili kuepusha uvujaji wa taarifa, jina lake lingekuwapo kwenye taarifa angeweza kujua na kusitisha utekelezaji aliokuwa kapanga kufanya na wenzake.
"Agosti 6 mwaka 2020, Afande Kingai alinipigia simu akaniambia kuna watuhumiwa wawili wamekamatwa Moshi, Agosti 7 niliitwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, nilipofika niliwakuta kina Afande Kingai nje," alidai.
Alidai kuwa alipokea simu za washtakiwa kutoka kwa Koplo Goodluck Minja, alikabidhiwa maelezo ya mashahidi, hati ya kukamata mali lakini watuhumiwa hakuwaona.
Shahidi alidai Afande Kingai alimkabidhi maelezo ya onyo ya Adamu Kasekwa na Afande Jumanne alimkabidhi maelezo ya onyo ya Mohammed Ling'wenya ambapo vitu vyote alivyokabidhiwa alihifadhi katika kabati la chuma lililopo Makao Makuu ndogo ya Upelelezi Dar ea Salaam.
Shahidi huyo alidai kuwa Agosti 8, 2020 waliwahamisha watuhumiwa, Kasekwa na Ling'wenya kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam na kuwapeleka Kituo cha Polisi Mbweni, Afande Jumanne akawakabidhi chumba cha mashtaka kisha wakaondoka.
Inspekta Swila alidai alionana na Luteni Urio ofisini kwake Agosti 11, 2020 na alichukua maelezo yake, akieleza mawasiliano yake na Mbowe kupitia mtandao wa telegram.
Alidai Urio alitaja namba walizokuwa wakiwasiliana za Mbowe 0719 933386, 0784 779944 na namba za Luteni Urio 0787 555200 na 0754 612518.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, Halfani Bwire, Adamu Kasekwa na Mohammed Ling'wenya ambao wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya kula njama kufanya vitendo vya kigaidi.