MOHAMED SAID: Alifungwa Enzi za Nyerere, Asamehewa na Rais Samia- Part 2



Pamoja na imani yake kuongezeka Mohamed alikuwa amekata tamaa ya kuishi, hivyo wakati wote akiwa gerezani hakutaka kujifunza ujuzi wowote akiamini hatoweza kuutumia kwa sababu kilicho mbele yake ni kunyongwa hadi kufa.

Hilo likamfanya ajikite kwenye shughuli anazopangiwa kila siku, lakini si kutafuta ujuzi ambao ungemfanya kubobea kwenye eneo fulani kama ambavyo wafungwa wengine hufanya mfano ujenzi, ufundi seremala, shughuli za kiwandani.

Anasema wakiwa gerezani walikuwa wanapata wasaa wa kusikiliza redio na televisheni, hivyo walikuwa wakifahamu masuala mbalimbali yalikuwa yakiendelea ndani na nje ya nchi.

Kifungo chake hakikuishia Ukonga, kwani katika kipindi cha miaka 30 baada ya kuhukumiwa alihamishwa kwenye magereza kadhaa ikiwemo la Dodoma, Tanga alikokaa miaka 22 na hatimaye akarejea tena Ukonga.


Siku moja katika kusikiliza habari kwenye redio wakapata taarifa kuwa adhabu ya kunyongwa imefutwa na Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini makubaliano ya kuzuia adhabu hiyo.

“Ilikuwa habari njema kwa tuliokuwa na adhabu ya kunyongwa nakumbuka ilikuwa wakati wa Rais Benjamin Mkapa, hilo jambo siwezi kusahau tulishukuru na kumuombea dua kwa Mungu ampe afya njema maana ametunusuru kwenye kifo, lakini bado tukawa na wasiwasi kwamba akija Rais mwingine itakuwaje.

“Basi niliendelea kukaa gerezani hadi mwaka 2005 ndipo nilipopewa taarifa rasmi kuwa adhabu imebadilishwa, imetoka kwenye kunyongwa hadi kifungo cha maisha, ilinipa matumaini kiasi fulani, lakini bado huwezi kufurahia kwa kuwa upo gerezani sehemu ambayo hauna uhuru,” anaeleza.


Hata hivyo, ile hofu ya kunyongwa ikawa imeondoka, akaielekeza akili yake kuamini kuwa maisha yake yote yatakuwa gerezani hivyo akalazimika kukubaliana na maisha ya gerezani na kufanya kila kinachotakiwa kufanyika.

“Kabla ya kuingia jeshini nilikuwa mchezaji na sisi ndio tulianzisha timu ya Simba B, nilipokuwa gerezani nikarudi kucheza mpira na kule tukawa na timu kabisa Simba na Yanga, tukawa tunajipa burudani kwa mtindo huo kujipotezea mawazo.

“Haikushia kucheza tu, tulikuwa mashabiki kindaki ndaki mpira ukichezwa huku uraiani na sie kule tunakuwa na presha kama ilivyo huku, kwa kifupi tulikuwa mashabiki hasa na wakati mwingine tulikuwa tunaandika barua kwenye klabu zetu na walikuwa wanatuletea misaada,” anasema.

Mwishoni mwa mwaka jana, alipata taarifa huenda akawa kwenye orodha ya wafungwa watakaosamehewa baada ya kutumikia kifungo chake kwa muda mrefu, habari hiyo aliifurahia lakini ilimpa mawazo.


Anasema hofu yake kubwa ilikuwa kuanza maisha ya uraiani, hakujua wapi aanzie na watu wake wa karibu wengi wameshafariki dunia, hivyo alijua anakwenda kukumbana na upweke na mahangaiko.

Hata hivyo, alijipa moyo na kujifariji ni bora maisha ya upweke akiwa huru kuliko kuendelea kukaa gerezani, hivyo kwa mara nyingine akamuomba Mungu amuonyeshe njia ya kuweza kuishi maisha mapya.

Maisha mapya uraiani

Desemba 9, 2021 siku ambayo Tanzania iliadhimisha miaka 60 ya Uhuru, Mohamed ni miongoni mwa waliofurahia siku hiyo kupita kiasi.

Ni siku ambayo alitoa mguu wake nje ya geti la Ukonga akiwa huru ikiwa ni baada ya kupita miaka 40 tangu awe katika hali hiyo.


Mohamed anasema mabadiliko aliyoyaona nje akatambua kuwa hawezi kufika popote kutokana na ugeni aliokuwa nao, hivyo akampigia simu rafiki yake ambaye alikuwa na namba zake.

“Alikuja kunifuata pale nikaenda kwake nikiwa najipanga kuwatafuta ndugu zangu au watu niliokuwa na uhusiano nao, maana nilivyotoka gerezani nimekuta wengi wamefariki dunia na hata maisha yamebadilika.

“Baba, mama, dada, kaka wote wamefariki, nyumba yetu iliyokuwa Temeke nimekuta ilishauzwa sijafanikiwa kukutana na ndugu yeyote. Hadi sasa naishi kwa msaada wa mtu ambaye kwa sasa namchukulia kama ndugu yangu,” anasema.

Kulingana na Mohamed, wakati anakamatwa alikuwa na watoto wawili, lakini kufungwa kwake kulimfanya apotezane nao na baadaye alipata taarifa za mtoto mmoja.

Anasema, “Najihesabu sina mtoto, nilikuwa na watoto wawili, wa kiume alikuwa na miaka miwili kama sio mitatu wakati nakumbwa na madhira haya na wa kike alikuwa na mwezi mmoja.


“Watoto hawa kila mmoja alikuwa na mama yake, basi kufungwa kwangu kukafanya nipotezane nao ila huyu wa kike nilisikia yeye na mama yake aitwaye Asha Kipini walishafariki. Sina uhakika wa taarifa hizo kama yupo hai wanitafute walikuwa wanaishi Mwananyamala”.

Kama ilivyo kwa mtu mwingine ambaye hakuwepo nchini kwa muda mrefu, hamu kubwa ya mzee huyu ni kufika maeneo aliyokuwa akizunguka miaka hiyo ila changamoto anayokutana nayo ni mabadiliko makubwa yaliyotokea katika jiji la Dar es Salaam ndani ya miaka 40.

“Sijui kama Matunda Bar bado ipo, ila natamani siku moja niende Manzese nikaone yale mazingira, mambo mengi yamebadilika. Yaani hata nikitembea barabarani najiona niko tofauti na watu wengine, najaribu kujitahidi kuzoea mazingira ya nje. Niliacha simu za mezani, sasa nimekuta simu za mkononi, basi nashangaa vitu vingi kwangu ni vipya.

“Changamoto kubwa ni shughuli ya kufanya, katika umri huu siwezi kufanya kazi ngumu naomba kama kuna uwezekano wafadhili wanisaidie nipate eneo nifanye biashara ndogo ndogo, ili niweze kupunguza makali ya maisha, nimeona huwezi kuishi kwenye jiji hili ukiwa huna shughuli ya kufanya,” anasema.

Kwa atakayeguswa kumsaidia Mohamed Said anapatikana kwa 0654718896

Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad