Uongozi wa Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ Simba SC umekiri kupokea kwa mikono miwili Ratiba ya Robo Fainali ya Michuano hiyo, baada ya kupangwa mapema leo Jumatatu (Februari 21).
Simba SC imepangwa kukutana na Pamba FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kati ya April 08-13.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema, wakiwa mjini Niamey-Niger walifuatilia harakati zote za upangaji wa Ratiba ya Robo Fainali na wamepokea kwa mkono miwili walichopangiwa.
Amesema wanaiheshimu Pamba FC, na kwenye mchezo huo Simba SC itacheza kwa heshima zote kutokana na kuamini kuwa yoyote aliyetinga Robo Fainali ya ‘ASFC’ ana hadhi kubwa, licha ya utofauti wa madaraja wanayocheza.
“Tulikua tunafuatilia kila hatua ya upangaji wa michezo ya Robo Fainali tukiwa hapa Niamey, tumepokea kwa mikono miwili kilichofanyika, na tumemjua mpinzani wetu kwenye hatua hii ambayo tutakwenda kuicheza mwezi April.”
“Tunaiheshimu Pamba FC licha ya kuwa Daraja la Kwanza, dhumuni letu ni kucheza soka la upinzani na tunaamini mpinzani wetu atatupa changamoto katika mchezo huu ambao kwetu utakua muhimu kutokana na hitaji la kutetea ubingwa wetu.” Amesema Ahmed Ally.
Wakati Simba ikipangwa kukutana dhidi ya Pamba FC, Watani zao wa Jadi Young Africans wamepangwa kukutana na Geita Gold FC, huku Azam FC ikipangwa dhidi ya Polisi Tanzania.
Mchezo mwingine wa Robo Fainali utakua kati ya Kagera Sugar FC dhidi ya Coastal Union ambayo itakua nyumbani Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Wakati huo huo TFF kwa kushirikiana na Wadhamini wa michuano hiyo Azam Media, wametangaza Ratiba ya Michezo ya Nusu Fainali, ambapo Mshindi wa mchezo kati ya Simba SC dhidi ya Pamba FC atakutana na Mshindi wa Mchezo kati ya Young Africans dhidi ya Geita Gold.
Mchezo mwingine wa Nusu Fainali utakua kati ya Mshindi wa mchezo wa Azam FC dhidi ya Polisi Tanzania ambaye atacheza na Mshindi wa mchezo kati ya Coastal Union dhidi ya Kagera Sugar.
Michezo ya Robo Fainali imepangwa kuchezwa kati ya April 08 hadi 13.