MTOTO wa miaka 10 (jina limehifadhi) katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili (jina la shule linahifadhiwa) amechomwa moto sehemu za siri na mapajani na mjomba wake.
Mkuu wa Dawati la Jinsia, Inspekta Tiho Masatu, aliyabainisha hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake kuhusu matukio ya ukatili wa kijinsia.
Alisema kwa sasa matukio hayo yanaongezeka kila siku licha ya kuwapo juhudi mbalimbali za kutokomeza vitendo hivyo.
Masatu alisema tukio hilo la kinyama lilifanywa na mjomba wake ambaye ni mume wa shangazi wa mtoto huyo, aliyejulikana kwa jina la Ramadhani Ali Januari 20, mwaka huu na aligundulika kufanyiwa kitendo hicho na walimu wake.
“Mwendo wake na unyonge aliokuwa nao ndio sababu iliyofanya kumtambua kuwa amechomwa moto na mume wa shangazi yake. Matukio ya kikatili kwa sasa yameongezeka ndani ya jamii, lakini wanafamilia wanashindwa kutoa taarifa,”alisema Masatu.
Pia alisema mtoto huyo alichomwa moto kwa kutumia kisu ambacho alikuwa akikiweka katika moto na baada ya kupata moto kumchoma katika sehemu zake za siri na mapajani hali ambayo ilimsababishia maumivu makali na kushindwa kutembea vizuri.
Alisema shangazi wa na mtoto huyo alikuwa akifurahia kitendo alichofanyiwa mtoto huyo na mume wake kwa kuwa hawakutoa taarifa mahali popote juu ya ukatili huo.