Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema (Bazecha), Hashimu Issa (63) amesema alijua hakuwa na kesi ya msingi kutokana na waliomfungulia kesi hiyo ya jinai kushindwa kuiendesha.
Issa alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kuchapisha taarifa za uongo na kuzisambaza kwenye mtandao wa YouTube, katika kesi namba 179/2021.
Issa alikamatwa jana Jumatano Februari 23, 2022 na polisi muda mfupi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumfutia kesi ya jinai.
Baada ya kukamatwa alipelekwa Oysterbay kisha kituo kikuu cha Polisi alikoachiwa kwa dhamana.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Februari 23,2022 baada ya kuachiwa, Issa amesema tangu mwanzo alijua hakuna kesi ya msingi kutokana na waliomfungulia kesi kushindwa kuiendesha.
Amesema tangu kesi hiyo ifunguliwe Julai mwaka 2021 wamekuwa wakienda mahakamani bila kesi kuendelea.
“Cha kushangaza hata leo (jana) baada ya hakimu kuifuta wakati natoka nje ya chumba cha mahakama askari alinikamata na kuniweka chini ya ulinzi."
“Walinipeleka kituoni lakini badaye walipokuja mawakili wangu pamoja na viongozi wa chama waliniachia kwa dhamana bila kunieleza kosa langu,” amesema.