MZEE WA UPUPU: Kuna Mtoto Anachezeaga simu ya Mo Dewji Simba Ikifanya Vibaya?



Mara zote Simba inapopitia kipindi kigumu, mwekezaji wao Mo Dewji huibuka na maneno fulani ya mafumbo kupitia mitandao ya jamii. Hii huongeza taharuki kwa wana Simba ambao wakati huo wanahitaji faraja kutoka kwa mtu kama yeye.

Mafumbo ambayo huwa anatumia husababisha maswali mengi ambayo kila mtu huibuka na majibu yake na kuongeza sintofahamu. Baada ya kucheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara bila kufunga hata bao moja, wakipoteza mbili na suluhu moja, wazee wa klabu hiyo ambao kimsingi hawatambuliki kikatiba wakafanya kikao chao chini ya Hassan Dalali, mwenyekiti wa zamani wa Simba.

Siku hiyohiyo, Januari 30, 2022, Mo akaibuka na mafumbo kupitia mitandao ya kijamii. Alianza kwa kukiri kwamba hali si shwari ndani ya Simba. Kweli kuna tatizo!

Licha ya kubaini kwamba kuna shida klabuni, lakini akaonyesha kwamba hata yeye mwenyewe hajui shida hiyo iko wapi? Tatizo liko wapi?


Kama ilivyo kawaida yake, huwa hawezi kumaliza posti zake kuhusu Simba bila kuwakumbusha mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuhusu pesa anazotumia. Simba hii pesa hazina thamani. Hapa ni kama alikuwa akimaanisha kwamba kuna watu wanamdharau ndani ya klabu yao licha ya kuwa na pesa na kuzitoa kwa ajili ya maendeleo ya klabu.

Itakumbukwa kwamba siku chache zilizopita kulikuwa na taarifa kwamba Mo ndiye tajiri namba moja Tanzania, namba moja Afrika Mashariki na namba kumi na tano Afrika. Sasa tajiri kama huyu kudharauliwa na watu anaowazidi pesa kwa kiwango cha usingizi na kifo, ni tusi kubwa.

Mwisho kabisa akatoa wito wa kuhoji mchakato wa mabadiliko ulipofikia. Kwa heshima na taadhima tuulize transformation imekamilika? Mtiririko huu wa maoni ya Mo kupitia mitandao ya kijamii unaonyesha aidha kuna kitu hakiko sawa ndani ya Simba au ndani ya fikra zake mwenyewe kuhusiana na klabu hiyo.

Kitendo cha kila mara kuwakumbusha watu pesa anazotumia kwa ajili ya Simba huku akisema hapati faida, ni ishara kwamba pesa zake zinamuuma. Na kama kweli ishara hiyo inaakisi picha halisi, maana yake siku za Mo ndani ya Simba zinahesabika.

Mashabiki wa Simba wajiandae kisaikolojia. Siku yoyote watarajie kusikia ‘breaking news’ kwamba Mo kaachana na Simba. Mo amekuwa na tabia ya kuegemea kwa watu wa kuwalaumu kisha kujitoa pale anapohisi alilotarajia halijawa.

Hiki ndicho kilichotokea alipokuwa Singida United, timu ambayo aliibadilisha jina kutoka Mto Singida. Hiki ndicho kilichotokea alipokuwa African Lyon, timu ambayo aliibadilisha jina kutoka Mbagala Market. Mara zote alitafuta kichaka cha kujifichia na akatoka nduki kimoja. Sasa yuko Simba na dalili zimeshaanza kujitokeza.

Alijiuzulu kama mwenyekiti wa bodi baada tu ya kufungwa na Mtibwa Sugar kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi, Januari 2020. Katika mambo aliyoyataja ni pamoja na pesa anazotumia kwa ajili ya Simba. Akapigiwa magoti na kutengua uamuzi wake, lakini baadaye akajiuzulu tena na hakurudi.


Ameibuka tena kwenye mitandao na kuleta mjadala wa pesa. Hii inawaweka roho juu mashabiki na wanachama wa klabu hiyo ambao wamewekeza nyoyo zao klabuni. Ukimsikiliza mwenyewe anapoongea kuhusu Simba unapata hisia kwamba huyu jamaa ni Simba hasa na siyo mtu wa kutoka leo wala kesho.

Sasa kama hiyo ndiyo iko hivyo kweli, basi labda kuna mwanaye mmoja huchezea simu yake. Haiwezekani mtu mwenye mapenzi mema na Simba kiasi kile awe anayumbisha vichwa vya wana Simba wenzake wanaomtegemea. Na kama siyo mtoto kuchezea simu, basi akaunti yake imedukuliwa. Lakini binafsi naamini Mo anaelekea kuikimbia Simba, kwa hiyo anawaandaa kisaikolojia mashabiki wake

Mwanaspoti
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad