BAADA ya kushuhudia kikosi chake kikilazimishwa sare tasa nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema anabeba lawama zote kutokana na matokeo waliyoyapata dhidi ya Mbeya City kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hiyo ni sare ya tatu Yanga inapata msimu huu huku ikiwa haijapoteza mechi hata moja kati ya michezo 14 iliyocheza hadi sasa wakati huu ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 msimu huu.
Akizungumza na Nipashe baada ya mechi hiyo juzi, Nabi kwanza aliwapongeza wachezaji wake kwa sababu walipambana kutafuta matokeo, lakini akiisifu Mbeya City kwa kufanikiwa kuzuia mipango yao na kuondoka na pointi moja.
“Katika mchezo huu siwezi kumtupia lawama mchezaji yeyote na lawaza zote nitabeba mimi za kutopata pointi tatu kwa sababu mchezo ulikuwa mgumu, wachezaji walipambana kutafuta matokeo, lakini wapinzani wetu walikuwa mahiri na kuharibu mipango,” alisema Nabi.
Alisema timu zote hazikucheza vizuri kipindi cha kwanza na kipindi cha pili Yanga walicheza vizuri baada ya kubadilisha mfumo na kutengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia.
“Tulitoa wachezaji ambao hawakucheza nafasi zao kama Dickson Job aliyecheza winga nafasi ambayo si yake, hii ni kutokana na Yassin Mustafa na wengine kuwa majeruhi.
“Kuhusu Feisal Salum kutoanza si sababu ya kutopata matokeo, Mbeya City walicheza kwa kufika miguuni mwa wachezaji na kuziba katika njia,” alisema Nabi.
Alisema baada ya mchezo huo aliongea na wachezaji wake kwamba wasahau matokeo hayo na sasa wanaenda kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo huo kujiandaa na mechi ijayo.
Wakati Nabi akieleza hayo, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule, naye pia anawapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kurejea nyumbani na pointi muhimu dhidi ya wenyeji wao, Yanga.
Lule alisema aliwasoma Yanga na kuona jinsi wanavyocheza, hivyo kuhakikisha wanaingia uwanjani kuharibu mipango ya wapinzani wao hao jambo ambalo walifanikiwa.
“Tuliwaheshimu na tulianza na mfumo wa 4-4-2, lakini kila muda unavyosonga tukabadilisha mfumo na kuingia na 4-3-3, kwa kuhakikishia tunawakaba Khalid Aucho na Zawadi Mauya ambao walikuwa kati,” alisema Lule.
Alisema baada ya kufanikiwa kuwazuia nyota hao na kuifanya Yanga kutochocheza mpira wao na kuleta madhara langoni mwao, jambo ambalo walifanikiwa kuondoka na pointi muhimu licha ya kwamba mipango yao ilikuwa kubeba zote tatu.
“Niwapongeze wachezaji wangu kwa kufanya kile nilichowapa mazoezi na kukihamishia uwanjani, tuliwaheshimu Yanga kwa sababu wana wachezaji na benchi la ufundi zuri,” alisema kocha huyo na kudai kwamba Ligi ya Tanzania hakuna timu kubwa bali Simba na Yanga ni sawa na timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo.