Nape Nhauye "Ukikutana na Jiwe rudi nyuma, using’ang’ane kulipasua"



“Wakati mwingine safari ya mabadiliko sio rahisi sana, inaweza kuchukua muda, inapochukua muda haimanishi safari kuwa imesimama, ni rahisi kutuhumiana, wakati mwingine unaposonga mbele unaweza kukutana na jiwe, unapokutana na jiwe, using’ang’anie kupasua jiwe, rudi hatua moja nyuma nenda kushoto au kulia, lipishe jiwe unaendelea mbele.

“Ukirudi hatua moja haimanishi umeacha safari, unatafuta njia nzuri ya kuendelea na safari jiwe linaweza kushugulika na Mwenyezi Mungu baadae, linaweza kuyeyuka au kufanya nini…wanahabari wenzangu mnanielewa?....(kicheko) shida yenu mnacheka, hayo majina yana shida, lakini ujumbe wangu mmeuelewa, ninachotaka tuaminiane..” amesema Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye leo Alhamisi Februari 10, 2022 katika mkutano wa wahariri wa vyombo mbalimbali ya habari jijini Dar es Salaam.

Nape amesema mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu inataka ushirikiano na maelewano kati ya serikali na vyombo vya habari na kwamba kwa sasa wanapokea maoni ya wadau wa habari ili kufanyia marekebisho baadhi ya vifungu vya sheria ili ziwe rafiki kwa vyombo vya habari.

“Nataka tuboreshe mahusiano kati ya wanahabari na serikali, najua tulipotoka, tunatakiwa kufanya mabadiliko ya sheria, kanuni sera na taratibu, ili ziwe rafiki kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari.


“Na kwa kuanzia nimesema leo tukutane na wahariri, naagiza Idara ya Habari Maelezo, kwa kushirikiana na jukwaa la wahariri na wadau wengine kuandaa kikao cha wadau tuje tujadili mapendekezo ya sheria za wanahabari.

“Tufanye mapitio kifungu kwa kifungu kisha serikali tupeleke mapendekezo bungeni. Mimi nilisimamia sheria ile, mazingira ya wakati ule na sasa ni tofauti, mazingira ya 2016 na 2022 ni tofauti, ni maagizo ya Mheshimiwa Rais sheria na sisi kazi yetu ni kutekeleza.” amesema Nape

Hata hivyo ametadharisha mazungumzo hayo si kwamba sheria itasimama atakayekwenda kinyume hatosita kumchukulia hatua stahiki.


“Mazungumzo haya hayafanyi sheria isimame, hili lazima tukubaliane, yale yenye utata ambayo tukaweza kuyapa muda tutafanya hivyo mfano kiwango cha elimu tuongeze mwaka mmoja wakati huo tunazungumza….; “Hivi leo mwandishi wa habari mwenye miaka 50, 55 unampelekaje darasani alafu unamstaafisha mapema. Hili tutapitia.

Nape amesema haki za Waandishi wa Habari ni lazima ataendelea kuzipigania na kuhakikisha waandishi wanapata stahiki zao.

Aidha Nape amezielekeza taasisi zilizokuwa zinasita kutoa matangazo na kulipa madeni, zitoe matangazo kwa vyombo vyote vya habari kwa usawa bila upendeleo wala kubagua.

“Niwaombe wanahabari tuaminiane, mimi mwandishi wa habari mwenzenu. Hiki ninachokieleza ndicho kipo kwenye moyo wa Rais na uelekeo wa serikali ya awamu ya sita ni tufanye kazi kwa pamoja.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad