LEO Saa 4 usiku Afrika itasimama kushuhudia dakika 90 za mchezo wa fainali za Afcon 2022 kati ya wababe wawili Misri na Senegal. Kiuhalisia ni kwamba Leo sioni rekodi za nyuma zikifanya Kazi.
kikeke pic
SALIM KIKEKE, YAOUNDE
LEO Saa 4 usiku Afrika itasimama kushuhudia dakika 90 za mchezo wa fainali za Afcon 2022 kati ya wababe wawili Misri na Senegal. Kiuhalisia ni kwamba Leo sioni rekodi za nyuma zikifanya Kazi.
Kwa jinsi nilivyoziona timu hizi tangu siku ya kwanza tutegemee kitu Cha tofauti sana uwanjani.
Ni fainali inayohusisha sura nyingi za ushindani ikiwamo mbinu za makocha wa timu hizo kongwe na maarufu kwenye soka la Afrika.
Nimekuwa nikitangaza mubashara matangazo ya mpira kupitia BBC idhaa ya Kiswahili, lakini fainali ya leo naona itasheheni mbinu zaidi haswa kwa kocha wa Misri ambaye alishinda nusu fainali dhidi ya wenyeji Cameroon kwa mbinu nje ya uwanja zaidi.
Mtakumbuka kuwa Kocha wa Misri aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Man United enzi ya Sir Alex, nusu fainali alichokifanya ni kutumia mbinu za kuwavuruga wachezaji wa Cameroon na mwamuzi ndio sababu ya kupigwa kadi nyekundu.
Kilichoonekana zaidi ni wachezaji wa Misri kujiangusha wakiguswa kidogo, kupoteza muda na mpira huku kocha wao akimzonga mwamuzi kila wakati, hiyo ni mbinu hapo unapunguza kasi ya washindani na kuwaathiri kisaikolojia uwanjani. Sasa sijui ataingia na mbinu gani Leo.
Kuhusu Kocha wa Senegal, amekuwa na nyota nzuri na timu hiyo, mbinu nyingi na huwezi kumtabiri ataingia vipi. Kwa hiyo yeyote akifanya makosa ataadhibiwa na mshindani wake. Itakuwa mechi kali sana.
Sura nyingine ni ushindani mkubwa wa kutafuta heshima na rekodi kati ya Sadio Mane wa Senegal na Mohamed Salah wa Misri.
Wachezaji hao ni jamaa wa karibu wanaochezea Liverpool na wote wameonyesha kiwango kizuri tangu kuanza mashindano hatua za makundi.
Ndio wachezaji tegemeo katika timu zao na wako kwenye vita ya kugombea heshima nani ameweza Taifa lake kuchukua kombe. Kwa hiyo kila mmoja anaona kabeba mzigo mkubwa wa Taifa lake na ndio sababu huenda tukaona kiwango bora kabisa.
Kuhusu nje ya uwanja, hisia na mitazamo ya mashabiki iko katika presha kubwa. Kila shabiki pande hizi mbili anaona anastahili kuchukua kombe kwa hiyo ndio hali ilivyo.
Suala la rekodi sijui nani kamfunga mwenzake zaidi sidhani kama lina nafasi kubwa katika mchezo huu. Tunachotegemea ni umakini wa timu, mbinu za kocha na hali ya wachezaji.
Mapungufu yaliyoonekana
Changamoto zilizojitokeza ni ndogo sana licha ya malalamiko kadhaa kutoka kwa shabiki hususani waamuzi walivyochezesha mechi kadhaa tangu siku ya kwanza.
Kwa asilimia 90 naweza kusema uamuzi wa waamuzi ulikuwa sahihi japokuwa ni wanadamu pia. Tukio pekee nililoshangaa ni lile la mwamuzi kumaliza mchezo wa Tunisia kabla ya dakika 90, sijui kitu gani kilitokea.
Kuhusu kadi nyekundu, penati zilizotewa sijaona tatizo sana lakini unajua kila uamuzi kuna shabiki watautazama kama halali na wengine pia wataona haikuwa haki, hata kama tumeanza kutumia mashine za VAR bado mwamuzi ambaye ni binadamu ndio atakayeamua hatua ya mwisho.
Hata Ligi Kuu ya Uingereza bado kumekuwa na wasiwasi katika uamuzi licha ya kutumia VAR.
Upekee Afcon 2022
Mashindano haya kwa mara ya kwanza yametazamwa na watu wengi sana duniani ikilinganishwa na miaka iliyopita kutokana na kiashiria kimoja na haki za urushaji wa matangazo kupitia Kituo cha Sky.
Sky hawawezi kununua haki za kurusha matangazo youote bila kufanya utafiti, ndio wenye haki ya kurusha matangazo ya michezo inayotazamwa zaidi duniani kwa hiyo Sky imeifanya Afcon 2022 kutazamwa zaidi.
Utofauti pili umeonekana katika umakini wa Cameroon kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Uviko kwa wimbi la nne.
Kabla ya kutoka Uingereza nilipima, nikafika Uwanja wa Ndege Yaoundé nikapima. Pia siku moja kabla ya kwenda uwanjani lazima upime
Pamoja na kupima, lazima uonyeshe cheti ndio unaingia kuangalia mechi tena ukiwa umevaa barakoa kwa hiyo wamekuwa makini sana Cameroon, imeonyesha utofauti sana na Afcon zilizopita.
Tanzania inaweza kuandaa Afcon
Uzoefu wangu katika mashindano haya kuanzia ubora wa viwanja vya Cameroon, huduma za hoteli na mazingira unanipa ujasiri wa kuamini Tanzania inaweza kuandaa mashindano hayo kwa miaka kadhaa ijayo.
Ukiangalia hapa Cameroon wanao uwanja mmoja tu mkubwa wenye hadhi kama ule wetu wa Benjamini Mkapa, uzoefu wa kupokea wageni Tanzania tuko vizuri kupitia shughuli za utalii, sioni sababu ya kushindwa sisi.
Labda ubora wa timu ndio wametuzidi lakini sifa nyingine zote tunazo, hata ikiwezekana Nchi za Afrika Mashariki zinaweza kuungana kuandaa mashindano haya kama ilivyokuwa Kombe la Dunia maandalizi ya kimkakati yanahitajika ambayo yatahusisha uwekezaji wa fedha na ushirikiano kati ya wadau, serikali.
Huku Cameroon kila baada ya eneo unakuta kuna akademi tena kuna mtu kajitolea kufundisha watoto bure halafu wazazi wa eneo hilo wanachangia gharama za kumwezesha.
“Sisi Tanzania sijaliona hilo, ni muhimu sana. Lakini pia maeneo ya wazi. Naona kasi yetu ni ndogo kukuza soka la mtaani. Timu zinaadaliwa mapema. Kwa hiyo Serikali na wadau washirikiane kuweka mkakati kuhakikisha tunawekeza maeneo hayo.
Tukutane usiku kwenye fainali ya kibabe. Kesho usikose uchambuzi mwingine wa fainali hapahapa kwenye Mwanaspoti na BBC idhaa ya Kiswahili.