Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya leo Alhamisi Februari 3, 2022 ameieleza mahakama kuwa amefunga ndoa na Jesca Nassari mwaka 2018 katika kanisa la Arusha Seven Day Adventist.
Sabaya ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hati ya makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha akiwa na wenzake, anaendelea na kesi makosa ya uhujumu uchumi akiwa na wenzake sita na sasa kesi hiyo ipo kwenye hatua ya utetezi baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.
Akihojiwa na mawakili wa Jamuhuri, Sabaya amesema amefunga ndoa Mei 27, 2018 na kwamba hakupelekea uthibitisho wowote mahakamani hapo, akisema yeye ndiye huo uthibitisho.
Sehemu ya mahojiano baina ya mawakili wa Jamuhuri na Sabaya
Wakili Neema: Wakati ukitoa ushahidi wako umesema umeoa je umeoa mwaka gani
Sabaya: 2018
Wakili: Nani jina la mke wako.
Sabaya: Jesca Nassari.
Wakili: Mlifunga ndoa lini na wapi.
Sabaya: Ndoa tulifunga kanisa Arusha Seven Day Adventist church 27/5 /2018
Wakili:Wasimamizi wa ndoa walikuwa kina nani.
Sabaya: Elibariki Nnko na Ruth Urassa
Wakili:Unasema ulioa je ulileta uthibitisho wowote mahakamani?
Sabaya: Sijaleta mimi ndio uthibitisho
Wakili: Siku hiyo na tarehe hiyo ulisaini nyaraka kuwa jambo ambalo lilifanya lipo kisheria je ni sahihi.
Sabaya:Ni Sahihi
Wakili: Wakati ukitoa ushahidi ulisema ulikamatwa 27/5/2021
Sabaya: Ni sahihi
Wakili: Wewe ulikuwa miongoni mwa wateule Rais ni sahihi .
Sabaya: Ndio.
Wakili:Uliteuliwa kama mkuu wa wilaya
Sabaya:Ndio.
Wakili:Unakubaliana na mimi kuwa uliapa kiapo.
Sabaya:Ndio niliapa
Wakili:Unakubaliana na mimi kwamba hakuna mtanzania yupo juu ya sheria .
Sabaya:Ndio
Wakili Mtenga:Naomba nianzie kwenye ndoa yako Jesca alisema cheti chake cha ndoa kipo nyumbani.
Sabaya:Jesca alisema ni cha kwake.
Wakili: Wewe cheti chako kipo wapi
Sabaya: Kipo kwangu.
Wakili: Sio nyumba moja na Jesca
Sabaya: Kipo nyumba moja ila kwenye eneo ambalo mimi nimehifadhi.
Wakili: Hujaona umuhimu wa kukileta hapa mahakamani.
Sabaya: Sijaona kwani sina shitaka la ndoa hapa.
Wakili: Uliwahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM mkoa Arusha.
Sabaya: Ndio
Soma zaidi:Mke wa Sabaya amaliza kutoa ushahidi kesi ikiahirishwa kwa muda
Kesi hiyo itaendelea kesho ambapo Sabaya ataendelea kuhojiwa na mawakili wa Jamuhuri.