Moshi/Mwanza/Dodoma. Ni kama Mbunge wa Kuteuliwa, Humphrey Polepole ameliamsha dude tena baada ya kuhoji ukimya wa mawaziri kutojitoa katika kundi ambalo Rais Samia Suluhu alisema wanakula zaidi ya urefu wa kamba yao.
Polepole ambaye amewahi kuhudumu kama Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, amedai mawaziri wa aina hiyo wamekosa uadilifu na hawana uhalali wa kuwataka Watanzania waishi maisha ya uadilifu.
Mwanasiasa huyo ambaye hivi karibuni amekuwa akipitia misukosuko kadhaa, ameyasema hayo kupitia video mbili alizozirusha katika ukurasa wake wa Twitter Januari 29, 2022 saa 3:03 na saa 3:39 asubuhi.
Katika video ya kwanza, Polepole aliandika “huwezi kuamini atakuja mtu hapa kunipinga. Kataa wahuni kwa nguvu zote” na ya pili akaandika “Asante Mungu na washiriki shule inaendelea. Kazi ni moja, kuchapa kazi na kukataa wahuni.”
Msingi wa hoja ya Polepole ni kauli ya Rais Samia aliyoitoa wiki mbili zilizopita wakati akizungumza na mawaziri na naibu wao, kuwa haelewi kwa nini kunakuwa na migongano baina yao na makatibu wakuu.
Kwa siku za karibuni, Polepole amehojiwa na kamati ya maadili ya CCM kutokana na kauli zake na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikaifungia chaneli yake ya mtandaoni kupitia Youtube, kuhusu “Shule ya Uongozi”.
Wanaokula zaidi ya kamba
Kupitia video zake alizozirusha katika ukurasa wake wa Twitter, Polepole alisema alitarajia baada ya kauli hiyo ya Rais, mawaziri waadilifu wangejitokeza na kuwalaani wenzao wanaokula kwa urefu zaidi ya kamba yao kama Rais alivyowaumbua.
Polepole alisema mawaziri na viongozi ambao si waadilifu wanakosa uhalali wa kuwataka Watanzania waishi maisha ya uadilifu na kusema kuanzia sasa atakuwa anamuuliza waziri kama anakula kwa urefu wa kamba kabla ya kuongea naye.
“Vile Rais ameshatuambia siri kubwa kweli, mnatakiwa mshukuru kwamba wako watu wanakula kwa urefu wa kamba na wanavimbiwa. Wamekula wakapitiliza. Hawa watu wana uhalali wa kutuambia tuishi maisha ya uadlifu? alihoji.
“Wanapata wapi uhalali. Wapi? Hakuna. Kwa hiyo mimi siku hizi nitakuwa nawauliza na wewe unakula kwa urefu wa kamba usiniletee habari zako, tukujue kwanza kama wewe unakula kwa urefu wa kambaaa?
“Basi mie nilitegemea hata mawaziri wangelaani. Unanielewa? kwamba bwana tunalaani wenzetu ambao wanakula kwa urefu wa kamba tabia hii haikubaliki. Lakini kimya,” alisema Polepole katika darasa lake hilo la maarifa 2022.
“Mimi nilitegemea mngetoka kumuunga mkono Rais. Hakuna mtu amemuunga mkono Rais. Hakuna, ni unafiki mtupu. Kwa sababu gani, watu wengi wanaogopa kusema ukweli. Sasa si Rais ametoka mbele amesema...
“Uongozi wa uadilifu tafsiri yake ni kwamba tunataka tabia ya uadilifu ianze hapa juu na hii ndio tumekubaliana huu ndio uadilifu. Huwezi kumwambia mtu usifanye kitu kibaya kama na wewe unashiriki katika mambo mabaya. Huwezi kumwambia sile rushwa na wewe tumekuona jana unapokea rushwa. Huwezi kumkemea mtu kwa jambo fulani ambalo na wewe unalifanya kila siku,” alisisitiza Polepole.
Ni miiko ya uongozi
Akizungumza na Mwananchi Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga alisema viongozi ni lazima waongoze kwa kufuata na kuishi miiko na viapo vyao.
Ni kutokana na umuhimu wa miiko na maadili, ndio maana Rais Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM amekuwa akiwasisitizia wateule wake kutovuka mipaka ya stahiki na halali yao kwa mujibu wa miiko, maadili na viapo vyao.
“Kwa mfano, ahadi za mwanatanu na baadaye CCM ya kutotumia cheo kwa masilahi na manufaa binafsi ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo kila kiongozi anayekasimiwa madaraka lazima azingatie na sisi kwenye chama tunakumbushia hilo kila wakati,” alisema Lubinga.
Alisema viongozi wa Serikali ambao wamepata nafasi zao kupitia dhamana ya CCM ni lazima waishi na kuongoza kwa kuzingatia miiko, ahadi za mwanachama na viapo vyao ndipo lengo la kuwaĺetea wananchi maendeleo kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi litafikiwa.
“Kuna haki na stahiki ambazo viongozi wanapewa kulingana na nafasi na vyeo vyao kwa mujibu wa kanuni na taratibu; ni lazima waishi kwa kuzingatia hilo maana kinyume cha hapo siyo tu ni kukiuka kiapo, bali pia maadili na miiko ya uongozi,” alisisitiza Lubinga.
Aliongeza; “Kutokana na umuhimu wa viongozi kuishi kwa kufuata na kuzingatia miiko, maadili na viapo vyao ndio maana hata Rais Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM amekuwa akiwasisitizia wateule wake kutovuka mipaka ya stahiki na halali yao kwa mujibu wa miiko, maadili na viapo vyao.”
Wasivuke mpaka wakavimbiwa
Akielezea mitazamo tofauti juu ya kauli hiyo, Professa Moh’d Makame Haji, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) alisema kauli ya Rais Samia si kwamba inahalalisha mazingira ya rushwa, bali imeweka mkazo wa kuzingatia masilahi ya mawaziri kisheria.
“Kwa tafsiri pana kwa watu wa Pwani, kwanza ‘urefu wa kamba’ maana yake ni kutovuka mipaka yako ya kimamlaka, sasa kula kwa urefu wa kamba yako, haimaanishi kujitengeneza mazingira ya kujipatia kitu nje ya mapato halali kisheria, lazima uzingatie mipaka na uhalali wa haki yako,” alisema Profesa Haji.
Kwa upande wake, Dk Richard Mbunda wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alifafanua kuwa kundi la wanaovimbiwa ni wale wanaokata kamba na kula nje ya posho, mishahara yao kikanuni na sheria za kazi.
“Kwa wanaovimbiwa ni kauli iliyoleta hisia kwa wananchi kwamba alitoa kauli za upole kwa wanaovimbiwa wakati Watanzania wamechoka sana na ubadhilifu, alitakiwa atoe kauli ya kimamlaka na kukemea au kuchukua hatua dhidi yao,”alisema Dk Mbunda.
Hata hivyo, Dk Wategere Kitojo wa Chuo Kikuu cha Arusha (UoA) alisema “kula kwa urefu wa kamba” “Ni tungo tata ndiyo maana ina mjadala kwenye jamii, hata mie nimeshindwa kutafsiri Rais alikuwa anamaanisha nini hasa,” alisema.