Polisi waanza utekelezaji agizo la Rais kuhusu kujitathmini
JESHI la Polisi limesema limepokea agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kulitaka kujitathmini utendaji wake na kwamba limeanza utekelezaji.
Juzi Rais Samia akizungumza na wananchi aliposimama wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza akiwa njiani kwenda Mara ambako jana alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za Maadhimisho ya Miaka 45 ya Kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma, aliliagiza jeshi hilo kujitafakari kutokana na baadhi ya askari wake kujihusisha na matukio ya mauaji na kisha kuona kama yanayotokea ndiyo misingi ya jeshi hilo au la.
Polisi wanatuhumiwa kufanya mauaji mkoani Mtwara Januari 5, mwaka huu na kusababisha maofisa saba wa jeshi hilo kushikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mkazi wa Kijiji cha Ruponda, wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi, Mussa Hamisi (25) aliyekuwa akiwadai askari hao zaidi ya Sh milioni 33.7.
Agizo la Rais Samia alilitoa baada ya Mbunge wa Magu, Boniventura Kiswaga (CCM) kumuomba kudhibiti mauaji yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo mkoani Mwanza, lakini pia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni kumweleza Rais kuwa Mwanza kulikuwa na matukio manne ya mauaji na wahusika tayari wametiwa mbaroni.
Kutokana na agizo hilo, HabariLEO jana lilizungumza na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, David Misime kuhusiana na utekelezaji na kueleza kuwa jeshi hilo limepokea na haraka limeshaanza kujipanga kuhakikisha linatathmini utendaji wake kwa ufanisi.
Alisema kati ya mambo ambayo jeshi hilo litazingatia katika kuhakikisha linajiimarisha ni kuchukua hatua za kinidhamu kwa askari wake wote wanaokwenda kinyume na miiko ya kazi za polisi.
Misime alisema pia litahakikisha linajipanga upya kiutendaji na ufanisi zaidi ili kuondoa kero na mambo ambayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya askari wake na ambayo yanawaathiri wananchi.
“Jeshi limepokea maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan na utekelezaji umeshaanza kuhakikisha linatathmini utendaji kazi wa askari wa jeshi hili pamoja na kuliboresha zaidi ili kuongeza ufanisi na muda si mrefu mtasikia nini kinafanyika,” alisema Misime.
Juzi Rais Samia alimweleza Masauni kuwa kuna mauaji yalitokea mkoani Mtwara na kwa taarifa alizonazo ni kwamba Jeshi la Polisi ndilo lilifanya mauaji hayo.
Alisema baada ya matukio hayo ya mauaji, Jeshi la Polisi likaunda kamati ya kufanya uchunguzi na kisha wamkabidhi taarifa (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi) jambo ambalo hakukubaliana nalo.
“Haiwezekani jeshi lifanye mauaji halafu lijichunguze lenyewe. Ndugu zangu wananchi na Watanzania, nimemwelekeza Waziri Mkuu aunde kamati nyingine iende ikafanye uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi halafu watuletee taarifa,” alisema Rais Samia.
Saa chache baada ya kauli hiyo ya Rais Samia, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza kuunda timu maalumu ya watu tisa ambayo imepewa jukumu la kuchunguza mauaji hayo ya Mtwara na Kilindi, Tanga. Kamati hiyo inatakiwa ikamilishe ripoti yake ndani ya siku 14.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wadau wamepongeza na kuunga mkono kauli na maamuzi ya Rais dhidi ya Jeshi la Polisi na tuhuma za mauaji.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania, Kajubi Mwakajanga alisema kitendo au agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka Jeshi la Polisi lijitafakari ina mantiki.
“Ni kitu kinacholeta mantiki, mtu hawezi kujichunguza yeye mwenyewe, kanuni za haki za binadamu zinakataa na nimeshangaa haya yote yakiendelea kutokea lakini wenzetu polisi hawajatoa msimamo wao hadi Rais ameingilia kati,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga alisema ni takwa la kisheria kwani kanuni haziruhusu.
“Ni uamuzi wa kupongezwa na kila wakati kwenye ripoti zetu tulikuwa tukiyaandika haya maana tunafanya kazi kwa ukaribu na polisi, hivyo agizo la Rais ni takwa la kisheria lipo katika Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania,” alisema Anna.
Imamu Mkuu wa Msikiti wa Tambaza na Shehe wa Kata ya Upanga Magharibi, Athuman Mohamed alisema agizo la Rais ni la busara juu ya kuundwa chombo cha kuchunguza ili kuja na suluhu ya mambo hayo.
“Mganga hajigangi, mkuu wa nchi akiagiza ni amri vyombo vinavyohusika vimemsikia Rais, tunatarajia utekelezaji hali ni mbaya hata sisi viongozi wa dini haitufurahishi kila kukicha unasikia huyu kanyongwa, yule kauawa ni tafrani juu ya tafrani Mungu atunusuru,” alisema Shehe Mohamed.