BONASI za wachezaji wa Simba kwenye michuano ya kimataifa zimepunguzwa, Mwanaspoti limejiridhisha. Msimu uliopita Simba ilitamba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika lakini msimu huu imeteleza na kunasa kwenye Shirikisho ambako mambo ni tofauti kidogo kuanzia kwa waandaaji mpaka klabu.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wachezaji wa Simba wakishinda ugenini walichukua Sh200 milioni kama bonasi walipotoka sare ugenini walivuta Sh100 milioni.
Mechi za nyumbani walikunja Sh100 milioni na sare walipewa Sh50 milioni. Uchunguzi wa Mwanaspoti umejiridhisha kwamba bonasi hizo msimu huu zimepunguzwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kiuchumi pamoja na fedha za mashindano husika.
Simba wakishinda nyumbani kama ilivyokuwa dhidi ya Asec Mimosas ni Sh60 milioni, wakitoka sare wanapata Sh30 milioni.
Wakishinda mechi ya ugenini wanapewa Sh100 milioni na sare Sh50 milioni. Habari za uhakika zinasema kwamba uongozi wa Simba umeshawaambia wachezaji kuhusiana na hilo na umeamua kufanya hivyo kutokana na zawadi kutoka kwa waandaji kuwa ndogo zaidi kwenye Shirikisho kulinganisha na Ligi ya Mabingwa.
Kama Simba watamaliza nafasi ya tatu au nne kwenye hatua ya makundi walipo sasa watapata Sh636milioni.
Robo fainali ya mashindano hayo watapata zaidi ya Sh809 milioni na kama wakisonga mbele zaidi ya hapo kama malengo yao yalivyo watapata mkwanja mrefu zaidi kutoka Shirikisho la soka Afrika (CAF).
MSIKIE MWENYEKITI
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu juu ya bonasi hizo kushushwa alisema; “Suala la bonasi la nini jamani mbona kuna mambo mengi ya kuandika, sio lazima mjue hilo ni siri yetu sisi, kama wewe hapo siri ya unachokipata ni wewe na mwajiri wako.”
Mangungu alisisitiza kuwa, jukumu la bonasi ni wao wanaamua kama uongozi hivyo hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuhoji juu ya hilo jambo ambalo halina tija na manufaa kwao lakini wameshakubaliana mambo yao ya ndani na wachezaji na morali iko juu.”