MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amewaita wanachama wa chama hicho waliokimbilia ACT-Wazalendo, warejee ili waweze kuchukua nafasi za uongozi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Mwenyekiti huyo wa CUF ametoa wito huo leo Jumamosi, tarehe 5 Februari 2022, katika hafla ya kuwapokea wanachama 33 waliorejea kutokea ACT-Wazalendo.
“Tunawaomba ndugu zetu wa visiwa vya Pemba na Unguja na wa Bara karibuni, mtakuwa na haki zenu katiba zinawalinda muweze kuchukua nafasi ya uongozi kwa kadri nyie wenyewe mnavyopendelea na namna wanachama wetu watawachagua tokea ngazi ya tawi, jimbo, wilaya hadi taifa,” amesema Prof. Lipumba.
Prof. Lipumba amewaita wanachama hao walioshusha tanga ACT-Wazalendo 2019 kufuatia mgogoro wa kiuongozi ulioibuka kati yake na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, warejee ili wakijenge chama chao.
“Tunawakaribisha tujenge chama imara, hali ya nchi yetu ni ngumu sisi ndiyo chama ambacho misingi na mizizi yake ni wanachama wa kawaida. Kuna vyama viko juu vinaweza kuwa na wenyeviti, makatibu wakuu na mabaraza ya juu lakini chini kwa wananchi wa kawaida hakipo,” amesema Prof. Lipumba.
Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF
Amesema chama chake kinahitaji watu wenye nia ya kudai tume huru ya uchaguzi na katiba mpya.
“Tunahitaji vijana wenye damu ya moto kudai haki, chama cha kuleta haki ni hiki. Tunahitaji watu wapambanaji na wazuri tuwape vijiti sababu lengo la kudai haki ni lengo ambalo bado Tanzania hatujaweza kulikamilisha, ni wajibu na ajenda ya kudumu tunapozungumzia haki tunazungumzia haki za kisiasa zinapatikana,” amesema Prof. Lipumba na kuongeza:
“Kupata katiba yenye misingi mizuri ya demokrasia, tunahitaji ule mchakato wa kupata katiba unauotokana na maoni ya wananchi wenyewe uweze kukamilika lakini vilevile ndani ya rasimu ya katiba ya warioba imeeleza msiingi mizuri ya kupatikana time huru ya uchaguzi sababu ni muhimu.”
Miongini mwa wanachama waliorejea CUF wakitokea ACT-Wazalendo ni Aliyewahi kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti ACT-Wazalendo Bara 2020, Juma Nkumbi.
Miongoni mwa sababu zilizowarudisha CUF zilizotajwa na wanachama hao ni kutoridhishwa na michakato ya uchaguzi ya ACT-Wazalendo.
Hata hivyo, chama hicho kimekanusha madai hayo.