Prof. Lipumba: "Nafasi yangu iko wazi"



MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa. Ibrahim Lipumba, amesema nafasi yake iko wazi kwa yeyote atakayetaka kugombea kwenye uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika mwaka huu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Prof. Lipumba ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, tarehe 12 Februari 2022, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

“Natoa wito na kuwahakikishia wanachama kwamba, hii nafasi ya mwenyekiti iko wazi kwenye uchaguzi unaokuja, kwa maana kwamba kila mmoja anaweza kugombea nafasi hiyo,” amesema Prof. Lipumba.

Mwenyekiti huyo wa CUF, amesema lengo la kutoa kauli hiyo ni kuonesha kuwa hajawahi kuwa kikwazo kwa watu kugombea nafasi hiyo na kwamba kila mwanachama wa chama hicho anayo nafasi ya kugombea nafasi za juu za uongozi.

“Nasisitiza vijana wajitokeze kugombea nafasi zote ikiwa ni pamoja na nafasi ya mwenyekiti wa Taifa, kwamba Lipumba hajawa na hatokuwa kikwazo kwa watu kujitokeza kugombea nafasi hizo,” amesema – Prof. Lipumba.

Aidha, Prof. Lipumba amesema anahitaji apate muda wa kukamilisha machapisho yake kuhusu ushiriki wake kwenye mapambano ya kudai haki, demokrasia na maendeleo ya uchumi wa Watanzania.

“Binafsi umri umekwenda Mingu akinijalia najitaji nipate muda wa kukamilisha machapisho ya ushiriki wangu katika mapambano ya kudai haki kwenye mapambano ya demokrasia na maendeleo ya uchumi wa Tanzania, wajibu wangu kuhakikisha chama kinakuwa imara na kupambana ili nchi yetu ipate haki,” amesema Prof. Lipumba.


Aidha, Prof. Lipumba amewaomba Watanzania waongeze ushiriki wao katika siasa ili wajenge demokrasia na vyama vya siasa vilivyo imara.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad