MBUNGE wa Ubungo jijini Dar es Salaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Kitila Mkumbo ameshauri kupitiwa na kupangwa upya kwa mfumo wa elimu nchini Tanzania kutokana na mfumo uliopo kwa sasa kuwa na mapungufu mengi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Profesa Kitila alisema hayo jana Alhamisi, tarehe 10 Februari 2022, wakati akichangia mfumo wa elimu nchini akisema haujasambaa upo “vertical” ambapo ikitokea mwanafunzi amekosea sehemu moja anajikuta ametoka kwenye mfumo hali ambayo husababisha upotevu wa wanafunzi.
Amesema badala ya kushughulikia changamoto za elimu nusunusu ipo haja ya kuupanga mfumo mzima.
“Tupitie na kuupanga mfumo wetu wa elimu na jambo hili siyo geni, mwaka 1982 Rais wa awamu ya kwanza Mwalimu Julius Nyerere aliunda Tume ya Makweta ambayo ilipitia mfumo wa elimu na kuja na suluhisho,” alisema Profesa Kitila
Profesa Kitila aliwashauri mawaziri wamshauri Rais Samia Suluhu Hassan aunde Tume ya Rais itakayopitia mfumo wote wa elimu na kuupanga upya.
“Jambo hili la kugusa tu mtaala wa msingi peke yake na sekondari peke yake, haiwezi kututoa, tunahitaji elimu ambayo itafiti Karne ya 21 na ambayo itatupeleka miaka 20 mingine ijayo na huu ni wakati muafaka maana dira yetu inaisha mwaka 2025 hivyo hii itatusaidia kwenda sambamba na dira yetu,” alisema Prof. Kitila.
Kuhusiana na upotevu wa wanafunzi, Profesa Kitila alitolea mfano wahitimu wa kidato cha IV mwaka 2021 ambao walianza shule ya msingi wakiwa 1,500,000 lakini walihitimu kidato cha IV wakiwa 483,820 ambapo zaidi ya watoto milioni 1 walipotea kwenye mfumo wakiwa na umri mdogo.
Amesema hata hao waliohitimu ni 173,000 tu sawa na asilimia 35.8 ya wahitimu wote ndiyo walifaulu kwa Daraja la I -III.
“Mwaka jana ofisi ya waziri mkuu wamefanya utafiti mzuri sana, waliita utafiti wa nguvu kazi ambao ulibaini Milioni 33 ya watanzania sawa na 54% ni nguvu kazi, 16% hawajawahi kwenda shule 65% wameishia darasa la saba na 15% wana elimu ya kidato cha IV,” alisema Profesa Kitila
Amesema ukitazama utafiti huo wa Ofisi ya Waziri Mkuu, utabaini umuhimu wa kuboresha mfumo wa Elimu nchini kwani nguvu kazi iliyopita kwenye mfumo wa Elimu bila stadi zozote ni 96% pekee na 4% ndiyo iliyopita katika mfumo wa Stadi.