BAADA ya Klabu ya Simba kumsimamisha winga wake, Bernard Morrison, kutokana na utovu wa nidhamu, kiongozi wa zamani wa klabu hiyo Ismail Aden Rage, ameunga mkono na kusema kama kuna wengine wapo kama mchezaji huyo waondolewe mara moja.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Rage alisema anawaunga mkono viongozi wa Simba kwa hatua waliochukua kwani klabu haiwezi kukaa na kumlipa mchezaji wa kigeni pesa za kigeni anayeshindwa kufuata masharti ya klabu.
"Naunga mkono kabisa, hatuwezi kukaa na wachezaji wa kigeni, tunamlipa pesa za kigeni, halafu hataki kufuata utaratibu wa klabu. Huo ni uamuzi sahihi na itakuwa ni fundisho kwa wengine," alisema Rage.
Kuhusu utovu wa nidhamu wa mchezaji huyo, Rage alisema hiyo ni hulka ya wachezaji wa Kiafrika anapoona yupo kwenye nchi ambayo ana soko na anapendwa na mashabiki wengi.
"Morrison ni mchezaji mzuri, ana uwezo, lakini isihalalishe kuwa ndiyo awe na nidhamu mbovu. Hii ni tabia ya wachezaji wengi wa Kiafrika hasa anapokuwa kwenye nchi ambayo ana soko na watu wanampenda, kwa Simba walichofanya ni sawa kwa sababu ikimwachia anaweza kuharibu tabia ya wachezaji wengine," alisema Rage.
Ijumaa jioni, klabu ya Simba ilitoa taarifa yake rasmi ya kumsimamisha mchezaji huyo kwa madai kuwa aliondoka kambini bila ruhusa ya uongozi na kwenda kusikojulikana.
Simba ilimsajili mchezaji huyo akitokea Yanga, na msimu huu anamalizia mkataba wake wa miaka miwili, huku taarifa za ndani zikidai kuwa klabu yake hiyo haitomwongeza mkataba, lakini tetesi zikidai huenda akarejea klabu yake ya zamani, Yanga.