Soko la Mbagala Rangitatu baada ya kuungua moto
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla amesisitiza umuhimu wa kutengeneza miundombinu ya njia kwenye masoko inayoweza kusaidia kukabiliana na majanga ya moto huku akisema amechoka kusikia ajali za moto katika mkoa huo.
Kauli hiyo ameitoa leo Februari 13, 2022, wakati anatoa pole kwa wafanyabishara wa Soko la Mbagala Rangitatu lililoungua kwa moto ulioanza kuwaka kuanzia saa 10:00 alfajiri ya kuamkia leo muda sawa na bweni la wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ilala Islamic lilipoanza kuungua.
Katika matukio hayo yote mawili yaliyotokea alfajiri hiyo ya kuamkia leo hakuna madhara kwa binadamu baada ya Jeshi la Zimamoto na uokoaji kuwahi na maeneo ya matukio na kuzima moto ambao hata hivyo umesababisha hasara kwa baadhi ya vitu kuteketea kwa moto.
Makalla amesema amechoka kusikia ajali za moto katika Mkoa wa Dar es Salaam kwani sababu zinazotolewa kuhusiana na matukio mengi zinafanana huku akiwataka viongozi wa masoko kushirikiana na wafanyabishara kuimarisha ulinzi.
"Niwape pole wote kwa ujumla Dar es salaam, hamjapata ajali ya moto peke yenu nyingine imetokea Shule ya Sekondari ya Islamic Ilala, huko pia licha ya kuungua kwa baadhi ya vitu hakuna madhara kwa binadamu.
"Kupitia masoko naomba wafanyabisha kwa kushirikiana na viongozi wenu kujijengea tabia ya kuimarisha ulinzi wenyewe kwani unaanzia kwenu, mimi nimechoka kusikia ajali za moto, wekeni miundombinu ya njia zinazopitika ili iwe rahisi kukabiliana na ajali kama hizi zinapotokea," amesema Makalla.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo amewaomba wafanyabishara hao kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho Kamati inaundwa kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kujua hasara iliyopatikana.
"Tunaomba muwe na subira kamati itafanya kazi yake kwa siku tatu kufanya uchunguzi wake pamoja na taratibu zingine za kuboresha soko Ili kuruhusu shughuli zingine kuendelea katika Soka hili," amesema Mwegelo
moto pic1
Amesema soko hilo lilikuwa na vizimba 388 na vibanda 20 ambavyo vimeungua,kwamba wanashukuru zimamoto waliwahi mapema na kusaidia kuokoa na walifanikiwa kutokana na miundombinu ya soko kuwa mizuri ikiwemo barabara zinazopitika.
Kamshina Msaidizi Mwandamizi wa Zimamoto Kinondoni, Christina Sunga alisema taarifa za kufungua Kwa moto walizipata kutoka Kwa walinzi wa soko hilo na walikuja na gari na kuanza Kazi ya kuuzima usilete madhara zaidi.
"Hali tuliyoikuta eneo la katikati ilikuwa mbaya sana, moto ulianzia na eneo la fremu kuzunguka eneo zinapozouzwa nguo ambalo limepata madhara makubwa kutokana na aina ya biashara, amesema Kamshina Christina
amesema ushirikiano walioupata kutoka vikosi vya bandari na watu binafsi waifanikiwa kuuzima moto huo Kwa haraka.
"Tunashukuru miundombinu ilikuwa wezeshi ikiwemo njia zinazopitika na maji yalikuwepo ya kutosha jumla tukikuwa na gari tatu kupambana na moto kwa kuzunguka soko lote,"amesema
Katibu wa Soko la Mbagala Rangi tatu, Frank Mapolu amesema moto huo ulianza saa 10 kasoro huku akieleza chanzo cha moto huo bado hakifahamiki.
"Japokuwa kulingana na maelezo ya walinzi wetu wa soko wanasema moto ulianzia kwenye kizimba cha kuuzia dagaa na kusambaa kwa haraka kwenye maeneo mengine ya soko,"amesema