Sababu Kuu zinazofanya Watu Wengi Kuwa na Maisha Magumu

 


Moja ya shauku walionayo watu wengi iwe katika maisha au biashara ni kutaka kufanikiwa. Kutaka kupata mafanikio yawe ya kiuchumi,kiafya, ki-uhusiano, kifedha,na hata kiroho ni moja ya malengo yanayotamaniwa na kila mmoja wetu. Lakini licha ya uwepo wa nia,shauku,na juhudi tunazoziweka ili kuweza kuyafanikisha malengo hayo bado mambo yetu yanaonekana hayasongi. Kuna sababu kadha wa kadha zinazopeleka wengi kushindwa kufanikiwa kaika maeneo hayo, ila katika makala yetu ya leo tutaangalia na kujifunza sababu zinazopeleka wengi kutofanikiwa kuinuka kiuchumi. Hivi umekwishawahi kujiuliza, ni sababu gani zinazowafanya wengi wasiinuke kiuchumi? . kuna sababu kadha wa kadha za wengi kutoikuinuka kiuchumi.

Na baadhi ya sababu hizo ni kama zifuatazo:


1. Kukosekana kwa maarifa


Kuna nukuu fulani katika biblia isemayo kwamba “ watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa”. Msingi namba moja wa mafanikio katika nyanja yoyote ile kaika maisha ni maarifa. Maarifa ni ile njia inayotumiwa katika kujitoa katika shida ama kuweza kupata kitu au hekima.Na kukosekana huko kwa maarifa miongoni mwa watu wengi ndiko kwa kiasi kikubwa hupeleka wengi kutokuinuka kiuchumi. Na kwa maana hiyo, ili kuweza kufanikiwa katika nyanja yoyote ile katika maisha unahiaji kwanza kuwa na maarifa. Na maarifa hayo yanaweza kupatikana kwa kutumia njia kadha wa kadha kama vile kujisomea vitabu, kuwa na mshauri, kuhudhuria semina n.k. Kwa kujipatia kwako maarifa kwa namna moja au nyingine kutakusaidia katika kufungua hazina zilizositilika kichwani mwako na ambazo ikiwa zitatumika kimadhubuti basi zinaweza kukuinua kibinadamu, kiuchumi,ki-uhusiano, na kiroho.


2. Kutokutumia maarifa tuliyonayo


Hakuna jambo lililo gumu katika maisha kama nidhamu binafsi, nidhamu binafsi ni ile hali ya kujiwezesha kufanya kile unachopaswa kufanya hata kama haujisikii kufanya. Wengi wetu tunajua kile tunachopaswa kufanya ila kwa namna moja ama nyingine tunashindwa kufanya. Kujipatia kwako maarifa na kisha kutokufanyia kazi maarifa ulionayo ni sawa na kazi bure. Mafanikio katika maisha huwa hayategemei sana kiasi cha elimu au fedha ulizonazo. Mafanikio katika maisha huwa yanategemea uharaka wa kujipatia maarifa mapya mazuri na wepesi wa kuyatumia, ila wengi wetu kwa kutokulitambua hili tumekuwa tukikazana katika kujiongeza maarifa bila ya kuwa na utahayari wa kuyatumia maarifa hayo. Kuna nukuu fulani katika biblia isemayo kwamba” jiangalieni basi jinsi msikiavo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa,na yule asiyekuwa na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anachodhaniwa kuwa nacho”. Na nukuu hiyo ina maana kwamba; kubali kujipatia maarifa ,yatumie kuwanufaisha wengine,usipoyatumia yatayeyuka. Ni muhimu ukajipatia maarifa na kuyatumia maarifa hayo.


3. Matumizi mabaya ya muda


Kila mmoja wetu ana masaa ishirini na nne kwa siku,na jinsi unavyoyatumia masaa hayo ndiko kunakoweza kuleta kufanikiwa au kushindwa kwako.Muda ni rasiliamli ya muhimu sana.Muda ni rasiliamli ya pekee isiyoweza kurudi wakati inapotumika. Swali la muhimu unalopaswa kujiuliza ni kwamba; je,unautumia vipi muda wako?.uwekezaji wowote unaoufanya sasa kwa kutumia muda ulionao ndio utakachokuja kuvuna kesho. kamwe usikubali kutumia muda wako vibaya kwa kutokuwa na hiki au kile. Anza na matumizi mazuri ya muda pamoja na akili yako,na mungu atafungua njia ya kile usichonacho sasa. Ila wengi wetu kwa kutokulitambua hili tumekuwa tukiutumia muda wetu katika mambo kadha wa kadha ambayo kwa namna moja au nyingine yanakuwa hayana manufaa kwetu.


4. Matumizi mabaya ya pesa


Moja ya elimu ya muhimu sana na inayopaswa kuzingatiwa na kila mmoja wetu ni elimu ya fedha. Na kwa bahati mbaya elimu hii huwa haifundishwi darasani. Kukosekana kwa elimu ya misingi ya fedha ndio kunakosababisha wengi kuwa na matumizi mabaya ya pesa. Tatizo tulilonalo wengi sio upatikanaji wa fedha bali ni usimamizi bora wa fedha.Kupata fedha ni jambo rahisi kwani fedha huwa inapatikana kulingana na kiasi cha thamani unachokitoa kwa wengine, ili uwe huru kifedha, ondoa au punguza kero za mahitaji ya wengine.Na kwa kufanya hivyo watu watakupa pesa zao na utakuwa huru kukamilisha mahitaji yako yote. lakini licha ya hilo, suala la kusimamia kimadhubuti kile tunachokipata bado limekuwa ni tatizo. Kukosekana kwa usimamizi mzuri wa fedha ndiko kunakosababisha wengi wetu kutokuinuka kiuchumi kutokana na uwepo wa matumizi mabaya ya pesa. Ni muhimu tukajifunza jinsi ya kusimamia na kutumia fedha zetu vizuri.


5. Kutafuta pesa ndio lengo la kwanza


Kama nilivyosema hapo awali kwamba: ili uweze kuwa huru kifedha, basi ondoa au punguza kero za mahitaji ya wengine. na kwa kufanya hivyo watu watakupa pesa zao na utakuwa huru kukamilisha mahitaji yako yote.ila wengi wetu kwa kutambua ama kutokutambua tumekuwa tukiiweka fedha kuwa lengo letu la kwanza. Na katika kujifunza kwangu kuhusiana na maendeleo binafsi nilichokuja kujifunza ni kwamba; utajiri ni kupata unachokitaka na umaskini ni kukosa unachokitaka.Ukipenda kuhudumia watu kwanza utainuka haraka.maarifa ya kupenda kuhudumia watu yatakuwezesha kuona kile ambacho wengine hawaoni.


Yatakuwezesha kuona majibu na kero za watu.Na utatumia maarifa hayo katika ubunifu wa mbinu na huduma mpya.


Nakutakia utekelezaji mwema kwa kile ulichojifunza. 

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad