MSHITAKIWA wa kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi, Lengai Ole Sabaya (35) amemaliza kujitetea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kwa kudai kuwa ushahidi dhidi yake ni wa kisiasa.
Mbele ya Hakimu Patricia Kisinda, Sabaya alimaliza kutoa ushahidi Jumatatu akijibu maswali ya masahihisho kutoka kwa wakili wake, Mosses Mahuna.
Sabaya aliiomba mahakama isichukulie maanani ushahidi wa shahidi mmoja katika kesi hiyo kwa kuwa hauwezi kuthibitisha shitaka dhidi yake.
Alisema shahidi wa kwanza alidai hakuwa na taarifa rasmi ya Sabaya kuwepo jijini Arusha Januari 22 mwaka jana yeye na dereva wake aliyemtaja kwa jina moja la Kivuyo hivyo hakuona umuhimu wa yeye kumpeleka Katibu Tawala wa Wilaya ya Hai kuthibitisha hilo kama shahidi wa upande wa utetezi.
Sabaya alidai kuwa alishindwa kuandaa utetezi wake katika kesi hiyo kwa kuwa hati ya mashitaka ni batili kutokana na kuwa na utofauti na ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri na utofauti wa tarehe ya matukio, maeneo na kiasi cha utakatishaji fedha kinachotajwa.
Alidai kuwa kama vyombo vya dola vingefanya uchunguzi wangegundua kuwa mashitaka dhidi yake si ya kweli na kwamba vingegundua pia kwamba hata gari alinunua kwa vyanzo vyake vya mapato na hivyo wangetenda haki.
Akijibu maswali ya masahihisho kutoka kwa Wakili Mahuna, Sabaya alidai Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilikosea taratibu katika kesi hiyo ikiwemo ukamataji wake na kushikilia baadhi ya mali zake na za watu wengine kwamba ni kinyume cha sheria.
Alidai alikamatwa na kupekuliwa usiku kinyume cha sheria na kufananisha tukio hilo kuwa sawa na ujambazi. Alidai kuwa uthibitisho uko mahakamani kwa kuwa walipeleka gari bila utaratibu wa kisheria bila kuwa na hati ya ukamataji wa gari hilo na risiti.
Jana mahakama ilielezwa kuwa mawakili wa utetezi wana kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha hivyo waliomba tarehe ya mbali ya usikilizwaji wa kesi hiyo. Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Enock Mnkeni (41), Watson Mwahomange (27), John Aweyo (45), Syliverster Nyegu (26), Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31