Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu wa mwaka 2022, jijini Dodoma leo.
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee ameshauri Serikali kumaliza shauri la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa haki na kisheria.
Mdee ameyasema hayo leo Jumanne Februari 8, 2022, wakati akichangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu wa mwaka 2022.
Ameipongeza Serikali kwa kufanya mabadiliko katika muswada huo kwa kuwa awali ulivyokuja ulionekana kama kosa la ugaidi ni kosa la kawaida wakati ni kosa zito ambalo linamaumivu makubwa sana kwa watu.
Amesema kosa la ugaidi ni mpaka liwe la kutisha sana na lenye madhara makubwa sana kwa kutenda ama kutotenda, kwa kupanga au kwa kusiko kupanga.
Amesema sheria hiyo ya makosa ya ugaidi inaainisha kuwa ili liwe tukio la ugaidi makosa ya kiugaidi yana viashiria vyake.
Amekumbusha kuhusu shauri la mashehe wa uamsho ambao walikaa sana ndani kwa makosa ya ugaidi lakini ushahidi ukashindwa kupatikana.
“Leo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ana kesi, sitaki kuingilia lakini naamini kutokana na busara yako (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) na kutokana na vigezo ambavyo sheria hii imeainisha haya mambo muyamalize kwa haki na kisheria,”amesema.
Amesema kwasababu ugaidi sio suala la masihara na sio jambo la kitoto na kwamba ili liwe tukio la ugaidi linanaonyesha viashiria vya wazi vya madhara makubwa kwa mwananchi na jumuiya nyingine.
“Sheria zetu tuzitunge na kutejiekeza kwa kufahamu kuwa leo itamkamata Halima kesho Jenista (Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora). Na tukifanya mambo haya tutairahisishia mahakama kazi ili zideal (ishughulike) na kesi za maana,”amesema
Mwananchi