MVUTANO mkali umetokea kati ya pande mbili za wabunge wanaounga mkono hatua ya kupunguza watu ndani ya Mamlaka ya Hifadhi Eneo la Ngorongoro (NCAA) na wanaopinga uamuzi huo.
Aidha, wamemshauri Spika, Dk. Tulia Ackson, kuunda kamati teule kwenda kuchunguza jambo hilo.
Hayo yalijitokeza mwishoni mwa wiki wakati wa semina ya wabunge iliyoandaliwa na NCAA kwa maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Lulida, alisema aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi na Maliasili, iliyokwenda a na kukuta zinajengwa hoteli karibu na eneo la creta waliagiza ujenzi usiendelee.
Alisema wanaojenga nyumba za kudumu ndani ya hifadhi siyo wafugaji pekee, bali hata watumishi wastaafu wa hifadhi hiyo, na kwamba kuna maswali mengi kuwa wanatoa wapi vibali na vinaidhinishwa na nani, na ilipendekezwa waondolewe, lakini waliendelea kuwapo humo hadi sasa.
Naye Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa, alisema nchi ni kubwa watu wanaweza kupunguzwa na kupelekwa maeneo mengine, huku akihoji ukubwa wa kata zenye kijiji kimoja huku wakitumia zaidi ya Sh. bilioni 35 kupewa huduma zote muhimu.
“Wenzetu wa Ngorongoro kata moja ina kijiji kimoja, mimi nina kata yenye watu 27,000, wanapewa fedha kila mwaka, wanajengewa huduma zote muhimu za kijamii na bado watoto hawaendei shule wanafuga,” alisema.
Naye Mbunge wa Viti Maalum na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Hawa Bananga, alisema walipoenda walijikuta kwenye mazingira magumu kwa kuwa wanafuatiliwa kila walipokwenda na wakiongea tofauti na matakwa ya wenyeji wanakuwa kwenye hali ngumu.
“Ifike mahali serikali ifanye uamuzi, hali ni mbaya sana unapoingia tu unakutana na mifugo inaharibu mazingira, wanafuga kondoo ambao wanakula hadi mizizi na kung’oa uoto wa asili,” alisema.
“Leteni sheria bungeni tubadilishe, wapo waliotufuata wako tayari kuhama hata kesho, ila wanalazimishwa na wachache wanaonufaika kuendelea kukaa mle.”
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda, alisema kuna watu wachache wenye mifugo mle ndiyo wanashinikiza wengine kukataa kuondoka, ila baadhi wako tayari, hivyo ni bora ukaandaliwa utaratibu.
“Ukishazaa mtoto siyo mali yako bali ya Tanzania, kule tuna watoto hawasomi wanachunga mifugo tu, wanaonufaika watoto wao wanasoma shule nzuri na wanatibiwa Ulaya na Marekani,” alisema.
Naye Mbunge wa Kiteto, Edward Ole Kaita, alisema ni muhimu serikali ikaangalia sheria kwa kuwa haikusema idadi na hifadhi imepata sifa za kimataifa kwa kuwa na mchanganyiko wa binadamu na wanyama.
“Wanaozungumzia Ngorongoro wanaeleza upande mmoja wa wanyama, mifugo, watu na uharibifu wa mazingira hakuna aliyeeleza faida ya watu walioko mle. Mmeacha yamejengwa maghorofa na nyumba za bati nani katoa vibali?” Alihoji.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Asha Abdallah Juma, alisema ni muhimu serikali ikaharakisha kuleta Muswada wa Mabadiliko ya Sheria kwa kuwa hali ikiiachwa ilivyo urithi wa dunia utapotea.
Mbunge wa Korogwe, Timotheo Mzava, alisema Serengeti na Ngorongoro zinategemeana na unapoua mmoja lazima na mwingine afe, na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kuokoa maisha ya watu na maliasili.
Mbunge wa Simanjiro, Chrostopher Ole Sendeka, alisema “Hakuna anayekataa ongezeko la wananchi, lakini hakuna anayeeleza ongezeko la hoteli na camp ambazo zinachukua maji Creta.”
“Namwomba Spika aunde kamati teule iende Ngorongoro, Bunge lisifanye uamuzi wa upande mmoja. Sina tatizo watu kuhamishwa, ila lazima haki za binadamu zizingatiwe na tuelezwe kwanini watumishi wastaafu wa NCAA waliendelea kubaki na kujenga nyumba za kisasa na hawajachukuliwa hatua,” alisema.
Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Oleshangai, alisema ni muhimu wafugaji wakasikilizwa na kwamba wanaosema mifugo inatoka nje siyo kweli, huku akieleza kuwa tembo waliokufa walikula maboga eneo la Karatu, na kwamba kesi za ujangili zilizopo mahakamani ni za watumishi wa NCAA na siyo wafugaji.
“Serikali isikilize wananchi na siyo kupeleka vifaru, lazima tujadiliane. Kuna hoteli ndani ya creta inatuchukulia maji kwenye creta, tunataka mkiondoa watu na hizi hoteli mziondoe,” alisema.
Mbunge wa Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo, alisema mkataba wa UNESCO unataka kulinda binadamu na inapotokea mgogoro atalindwa binadamu, na pia ilani ya CCM inasema ikitokea mgogoro kati ya wanyama na binadamu haki ya binadamu italindwa.
“Hapa kuna mambo matatu tu yakufanyika ambayo ni kutumia mabavu kuwaondoa, kuwalipa fidia waondoke na kuwahamasisha waondoke kwa hiari. Kwanini serikali inashindwa kutumia mbinu hizi?”
Mbunge wa Viti Maalum, Ester Matiko, alisema inashangaza kuwa Baraza la Wafugaji lina nguvu kuliko serikali licha ya kuwa chini ya waziri na linapewa fedha na kuzitumia litakavyo huku walengwa hawanufaiki.
Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso, alisema Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilieleza namna mimea vamizi inamaliza malisho ya wanyama na mazalia ya nyumbu yalivyoharibiwa.
“NCAA inasomesha watoto hadi vyuo vikuu, mbona wa maeneo mengine hawasomeshwi, kila mara Manyara tunapokea wamama na watoto kutoka hifadhini wanakuja kuomba chakula kwasababu hali mbaya, fedha zinazotolewa zinamnufaisha nani?” Alihoji.
Mbunge wa Rorya, Hassan Chenya, alisema wananchi hao wanakosa haki za huduma za jamii zinazotolewa na serikali kwa sababu hawana pa kuzijenga na mara kadhaa wamepelekewa fedha, na kwamba ni aibu mbunge kuendelea kuongoza watu maskini, wasio na huduma za afya na mazingira magumu ya maisha.