BARCELONA, HISPANIA. GWIJI la soka la Cameroon, Samuel Eto’o amethibitishwa kuwa baba halali wa binti wa miaka 22 huko Madrid.
Straika huyo wa zamani wa Barcelona hakuwa anafahamu kama ni baba wa mrembo Erika Do Rosario Nieves na hakuhudhuria mahakamani wakati shauri lake lilipokuwa linasikilizwa huko Madrid.
Mahakama Namba 83 huko Madrid ilifikia uamuzi Alhamisi iliyopita na kukamilisha shauri hilo lililofunguliwa na mama wa binti huyo mwaka 2018. Mrembo Adileusa, ambaye ni mama wa Erika, alisema alikutana na Eto’o kwenye kumbi moja ya starehe za usiku huko Madrid mwaka 1997 wakati Mcamerooni huyo alipokuwa akiichezea Leganes, iliyopo karibu na mji huo mkuu wa Hispania.
Eto’o alitumikia msimu wa 1997/98 kwa mkopo huko Leganes akitokea Real Madrid, alifunga mabao manne katika mechi 30 kabla ya kurudi Bernabeu kwenda kupandishwa kikosi cha kwanza cha Los Blancos.
Kutokana na hilo la Eto’o kurudi Real Madrid, uhusiano wake na Adileusa ulishindwa kukua, lakini kwa mujibu wa shauri hilo ni kwamba mrembo huyo alijigundua kuwa ni mjamzito, Februari 1998. Kwenye shauri hilo ilielezwa kwamba Eto’o angeendelea kuwa na uhusiano mzuri na mwanamke huyo kama tu atakubali asimzae mtoto huyo. Na baada ya mwanamke huyo kubaki na ujauzito wake, Eto’o aliamua kukata mawasiliano na mrembo huyo, akigoma kupokea simu zake wala kujibu barua pepe.
Eto’o alidaiwa kuvunja mawasiliano na mama wa mrembo Erika, ambaye alizaliwa kwenye hospitali ya Alarcon Foundation, Madrid, 1999.
Kwa kipindi hicho, Eto’o alikuwa yupo Catalonia akiichezea Espanyol, alikojiunga kwa mkopo Real Madrid.
Eto’o inaelezwa kwamba hajawahi kuwapo mahakamani kwenye kesi hiyo na hakuwapo wakati wa kutoa uamuzi. Na kilichoamriwa ni kwamba Eto’o kumpa matumizi mwanaye kiasi cha Euro 1,400 kwa mwezi na anatakiwa kulipa kuanzia siku lilipofunguliwa shauri mwaka 2018.
Eto’o ni moja ya wanasoka waliopata mafanikio makubwa uwanjani na kuwa mmoja wa wanasoka mahiri wa Afrika. Alifunga mabao 70 kwa misimu yake minne aliyokuwa Real Mallorca kabla ya kwenda kung’ara Barcelona kati ya 2004 na 2009, akifunga mabao 130 katika mechi 199, akishinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Eto’o alikwenda kushinda taji jingine la Ligi ya Mabingwa Ulaya alipokwenda Inter, ambapo alifunga mabao 53 kwa misimu miwili aliyokuwa kwenye timu hiyo kabla ya kwenda Russia kujiunga na Anzhi Makhachkala.
Baadaye alijiunga na Chelsea, Everton, Sampdoria, Antalyaspor na Konyaspor, kabla ya kuhitimisha maisha yake ya soka Qatar SC