Serikali yatoa Tamko Vibali Ajira, Wastaafu



WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka utaratibu wa kupata watumishi katika kuziba mapengo ikiwa ni baada ya kupata takwimu sahihi za mahitaji.

Majaliwa ameyasema hayo jana bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga (CCM) wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Katika swali lake, Mtinga alisema: “Upungufu wa watumishi katika halmashauri zetu limekuwa tatizo kubwa sana, kwanini Serikali isianze kujaza nafasi zilizowazi mara moja pale mtumishi anapostaafu au anapotangulia mbele ya haki kwa sababu mtumishi yuko kwenye bajeti inayoendelea badala ya utaratibu wa sasa wa halmashauri kusubiri kuomba kibali cha ajira jambo ambalo linachukua muda mrefu na kuongeza ukubwa wa tatizo?”

Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema Serikali kupitia Wizara ya Utumishi imeweka utaratibu wa kupata watumishi katika kuziba mapengo ya watumishi kwa kutangaza ajira mpya.


“Lakini hili linafanyika baada ya kufanya uhakiki kwa vipindi vya miezi mitatu, miezi sita au mwaka mmoja kuona tuna upungufu wa watumishi kwa kiasi gani, wangapi na wakada ipi.”

Alisema Wizara kupitia Tume ya Utumishi imekuwa ikifanya uratibu wa wizara na idara zote kuangalia mahitaji. “Tunaweza kuona tunachelewa kutangaza ajira hizo kwa sababu lazima tupate takwimu ya pengo la watumishi na mahitaji kwa kutangaza mara moja.”

Wakati huohuo, Majaliwa alisema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaendelea kulipa mafao ya wastaafu na itahakikisha lengo la kulipa wastaafu kwa wakati linafikiwa. “Mabadiliko ya sheria yapo na kanuni zilishatengenezwa.


Kwa sasa tunaangalia kama kanuni hizi zitatuwezesha kulipa mafao ya wastaafu kwa wakati. Malengo yetu ni kulipa wastaafu wote kwa wakati na hatua hii tutaifikia.”

Majaliwa alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (Chadema) ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka bungeni Sheria ya Mifuko ya Jamii ili ifanyiwe tena mabadiliko na wastaafu waweze kupata amani kuhusu mafao yao na wasipate usumbufu.

Alisema mifuko hiyo ilikuwa mingi na serikali iliamua kuiunganisha ili ibakie michache ambapo kwa sasa kuna NSSF unaoshughulika na sekta ya binafsi na PSSSF ambao unashughulika na watumishi wa umma.

Alisema baada ya kuunganisha mifuko hiyo Serikali ilikuta kuna madeni mengi. “Sasa hivi tunataka tukamilishe ulipaji wa haya madeni ili tuanze kutoa mafao kwa wakati. Serikali iliwahi kutoa fedha ili kuiongezea nguvu mifuko ya hifadhi ili ikamilishe malipo yake kwa wastaafu.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad