Jana Shirikisho la Soka nchini TFF lilitangaza kumfungia Shaffih Dauda kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitano na faini ya TZS milioni 6.
Shaffih alipewa adhabu hiyo kwa kwenda kinyume na Kanuni za Maadili, na Kanuni za Utii za TFF. Kupitia kipindi cha Sports Xtra Clouds FM, Shaffih Dauda alizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu adhabu hiyo na kusema ameipokea na anajihisi hajafungiwa kwani atakuwa huru kuongea chochote
-
“Nimeipokea adhabu ya kufungiwa. Taarifa ambayo imetajwa iliandikwa kwenye ukurasa wangu wa Instagram na ilikuwa inazungumzia u-dictator wa shirikisho.Kama unakumbuka, baada ya GSM kuingia mkataba na TFF, baadaye TFF wakaja na barua ikipiga marufuku wadau kuhoji kuhusu mkataba ule. Atakayethubutu atachukuliwa hatua.
Baadaye GSM wakatoa barua ya kuvunja mkata na TFF. Baada ya hapo ndio likaandikwa andiko lililokuwa linazungumzia TFF kuzuia wadau kuhoji kuhusu masuala ya mkataba wao na GSM ambao baadaye GSM walitangaza kuuvunja.” alisema Dauda na kuendelea
-
“Kwa hiyo andiko langu lilikuwa linazungumzia kwamba TFF sio nyumba ya kupanga kwamba baba mwenye nyumba anaweza kuambua maji yatatoka muda fulani halafu bomba litafungwa. Unaweza kuwa umefungiwa lakini kumbe ndio upo huru zaidi. Hakuna vikwazo tena, kwa sababu hakuna vifungu vya kunizuia. Nitakuwa huru kuzungumza, kukosoa pale inapobidi ilimradi sivunji sheria. Sasa hivi nahisi sijafungiwa ila ndio nipo huru. Nilikuwa kwenye kifungo cha miaka mitano (5) sasa hivi ndio nipo huru.” - @shaffihdauda_