Shahidi wa 13 kufunguka mahakamani kesi ya Mbowe
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo itaanza kumsikiliza shahidi wa 13 wa upande wa mashitaka katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2021 ni makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Khalfani Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Ling'wenya.
Kesi hiyo iliyo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka sita ya kula njama kutenda vitendo vya kigaidi, ikiwamo kulipua vituo vya mafuta.
Kabla ya shahidi huyo wa 13, mahakama hiyo imemaliza kumsikiliza shahidi wa 12 ambaye ni Luteni Denis Urio aliyetumia siku tano kutoa ushahidi na kujibu maswali ya upande wa utetezi.
Luteni Urio ni ofisa JWTZ katika kikosi maalumu (makomandoo) kilichopo Ngerengere mkoani Morogoro.
Shahidi huyo ndiye aliyeibua tuhuma za njama za uhalifu zinazowakabili washitakiwa hao kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wakati huo, Robert Boaz.
Luteni Urio alidai mahakamani kuwa, alifahamiana na Mbowe mwaka 2008 wakati mwanasiasa huyo alipompigia simu na kujitambulisha kisha akamuuliza kuhusu wasifu wake na kumweleza kuwa wanatoka eneo moja, Moshi.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, tangu mwaka huo aliendelea kuwasiliana kwa simu na Mbowe ambaye alikuwa wakati mwingine akimtumia ujumbe wa kumtakia heri kuhusu matukio mbalimbali zikiwamo sikukuu.
Alidai katika mawasiliano yao, Mbowe alimwambia kuwa chama chake kimepanga kuchukua dola kwa namna yoyote hivyo alikuwa anahitaji wataalamu wa kufanya hivyo.
Alidai pamoja na kumpatia walinzi hao ambao walifukuzwa jeshini kutokana na vitendo vya kinidhamu, aliwashawishi kufanya vitendo vya kigaidi ikiwamo kwenda kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na baadaye walipue vituo vya mafuta Dar es Salaam.
Luteni Urio alikana kuwekwa kizuizini na kwamba mama yake mzazi hajawahi kwenda kumtembelea mahali walipomuweka wala hajawahi kupelekewa mtoto wake baada ya kuzaliwa.
Katika kesi hiyo, mawakili wanaoongoza kesi hiyo ni jopo la mawakili wa serikali waandamizi, Pius Hilla, Abdallah Chavula, Jenitreza Kitali, Nassoro Katuga, Esther Martin, Ignasi Mwinuka na Wakili wa Serikali, Tulimanywa Majige.
Mawakili wa utetezi katika kesi hiyo ni Peter Kibatala, Khadija Aron, Michael Mwangasa, Maria Mushi, Dickson Matata, Alex Massaba, Seleman Matauka, Michael Mwangasa na Nashon Nkungu.