Mahakama ya Hakimu Mkuu jijini Naironi, Kenya kwa mara ya pili imetoa agizo dhidi ya Katibu wa Ugatuzi Julius Korir kufika mahakamani siku ya wapendanao, Februari 14, kujibu mashtaka ya dhuluma.
Hakimu Mkuu Susan Shitubi alitoa wito huo baada ya wakili wake aliyekuwa jaji Nicolas Ombija kuiambia mahakama kwamba mteja wake alikuwa nje ya jiji la Nairobi kwa shughuli ya kikazi.
Kulingana na hati za mashtaka, katibu huyo alidaiwa kumpiga mkewe mjamzito Everlyne Chepkorir na kusababisha madhara ya kimwili.
Kwa mujibu wa shtaka hilo, anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 17, 2020 katika barabara ya Ndalat, nyumbani kwao Karen ikiwa ni kinyume cha sheria na kumdhuru mwilini na atakabiliwa na kifungo cha maisha iwapo atapatikana na hatia ya kumsababishia mkewe madhara.
Katibu wa Ugatuzi Julius Korir
Korir alikuwa ameelekea katika Mahakama ya Juu kusitisha kukamatwa kwake, ila hakimu Anthony Mrima mnamo Alhamisi, Novemba 11 alitupilia mbali ombi lake kwa msingi serikali ina haki katika kuendeleza mashtaka dhidi yake kwa kosa la kumpiga na kumjeruhi mkewe ambaye waliachana naye akiwa mjamzito.
Katibu huyo alikuwa amejaribu kuwazuia DPP na DCI kumkamata na kumfungulia mashtaka kuhusiana na kosa la jinai aliloliita kuwa ni kinyume cha sheria, kwa nia mbaya na kukiuka haki yake ya kikatiba akidai kuwa upande wa mashtaka ulikuwa unatumiwa kumshurutisha kutoa sehemu ya mali yake kuhusiana na mzozo wa ndoa.
Katibu huyo aidha, huenda akapoteza kazi yake kulingana na Sura ya 6 ya Katiba pamoja na Sheria ya Uongozi na Uadilifu inayosema “afisa yeyote wa serikali aliyeteuliwa atasimamishwa moja kwa moja endapo akashtakiwa kwa kesi ya jinai.”
Hati za mahakama zilionyesha kuwa mkewe aliripoti tukio la kushambuliwa katika Kituo cha Polisi cha Hardy huko Karen mnamo Novemba 20, 2018, chini ya OB 40/20/11/2018 na ripoti ya uchunguzi wa kimatibabu ya Novemba 20, 2018, ilifichua kuwa Koech alipata michubuko kwenye tumbo, mapajani na miguuni alipokuwa mjamzito na fomu ya P3, iliyotiwa saini na daktari wa upasuaji katika makao makuu ya polisi pia ilionyesha alikuwa na majeraha ya kifua na tumbo