UONGOZI wa Simba umesema kuwa hauna hofu kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast kesho Jumapili kutokana na maandalizi waliyoyafanya huku ukitoa onyo kali kwa wapinzani wao.
Simba inatarajiwa kuvaana na Asec ambayo aliwahi kuichezea beki mkongwe Pascal Wawa kutoka nchini humo, ambaye yeye anaijua vizuri timu hiyo.
Mchezo huo ambao ni wa kwanza wa hatua ya makundi ya michuano hiyo, unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Meneja wa Habari na Mahusiano wa Simba, Ahmed Ally, alisema wameshazijua mbinu watakazokuja nazo wapinzani kuelekea mchezo huo mgumu.
Ally alisema baada ya kuifutilia kwa karibu timu hiyo, walichogundua ni kwamba wanacheza soka la kujilinda ‘kupaki basi’ wanapocheza ugenini, hivyo hizo mbinu ndiyo zitakazowaharibia kwani zitawafanya wawapige bao nyingi.
Aliongeza kuwa wanajivunia uzoefu mkubwa walionao wa kucheza soka la Afrika, hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani kuisapoti timu yao watakapovaana dhidi ya Asec.
“Tunajivunia uzoefu tulionao hivi sasa wa kucheza soka la Afrika, hivyo hatuna hofu kuelekea pambano hilo na kikubwa niwatahadharishe hao Asec wanapokuja na mbinu za kupaki basi.
“Kama wakijipindua kucheza soka la kupaki basi, watarajie kula bao nyingi za kutosha kabla ya kurudiana nao. Nako huko nyumbani kwao wakijifanya wafunguke kucheza kwa kushambulia ndiyo watakuwa wamejichongea, tutawafunga nyingi zaidi tutakapocheza hapa nyumbani,” alisema Ally.