Simba Yastuka, Yahamisha Kambi Usiku Usiku



SIMBA wamepania. Katika kuhakikisha wanashinda mechi yao ya kwanza ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Asec Mimosas leo saa 10:00 jioni, uongozi umehakikisha wachezaji wanakuwa katika hali ya utulivu wa hali ya juu kwa kufanyia sapraizi ya kuwahamisha kambi.

Sapraizi hiyo ilikuwa baada ya kumaliza kula juzi saa 2:00 usiku walipewa tangazo kuwa wanatakiwa kuchukua kila watakachotumia katika mechi ya Jumapili kwani hawatalala kambini kwao hapo Mbweni na watahama.

Baada ya muda mfupi ziliingia gari mbili aina ya Toyota Coaster na kuwabeba wachezaji na benchi la ufundi na kuwapeleka katika hoteli ya Element by Westin Dar es Salaam, iliyopo Masaki pembezoni mwa bahari.

Msafara huo ulikuwa wa ukimya na usiri mkubwa huku wachezaji wakiwa katika mshangao kwani hawakuambiwa kinachoendelea ila walielezwa watakuwa katika hoteli hiyo mpaka watakapomalizana na Asec.


Msimu huu inakuwa mara ya pili Simba kuhama kambi kwani mara ya kwanza walifanya hivyo siku mbili kabla ya kucheza na Yanga katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Ligi Kuu Bara msimu huu.

Wachezaji wa Simba waliambiwa hakuna anayeruhusiwa kutoka nje ya hoteli hiyo, kumkaribisha mgeni yeyote.

Viongozi wa Simba katika kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 10:00 jioni, wamewaambia wachezaji kuwa wakishinda mechi hiyo ya Asec kabla ya kusafiri kwenda Niger watakuwa wamewawekea bonasi zao katika akaunti zao.


Kwenye mechi hiyo Simba itawakosa nyota wake sita, akiwamo Clatous Chama katika mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Asec Mimosas kwenye Uwanja wa Mkapa kesho, lakini kocha Pablo Franco anaamini kwamba wataifunga timu hiyo ya Ivory Coast.

Pamoja na Chama, Simba kesho katika mechi hiyo itawakosa Bernard Morrison, Taddeo Lwanga, Chris Mugalu, Hassan Dilunga na Kibu Denis kutokana na sababu mbalimbali.

Lakini kocha Pablo amesema ameandaa mbinu za kushinda mechi hiyo kibabe.

Kukosekana kwa mastaa hao kunamfanya Pablo abadili mfumo katika mechi hiyo na huenda akatumia mfumo wa 4-3-3, ambao ni tofauti na ule wa 4-2-3-1, ambao ulizoeleka kutumika chini yake tangu alipochukua mikoba ya kukinoa kikosi hicho. Hiyo ina maana ataanza na mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu.


Wachezaji ambao Pablo anaweza kuanza nao katika kikosi cha kwanza kesho ni Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Hennock Inonga, Jonas Mkude, Pape Osmane Sakho, Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere na Rally Bwalya.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad