Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameiagiza Serikali kutoa maelekezo ya jumla juu ya uharibifu wa barabara Nchini kufuatia vilio mbalimbali vya Wananchi kuhusu adha wanayokumbana nayo.
Dkt. Tulia ametoa agizo hilo leo katika kikao cha saba za bunge, akieleza kuwa wabunge wamekuwa wakipokea malalamiko kuhusu uharibifu wa barabara uliosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
“Serikali iseme jambo kwa sababu tunapigiwa sana simu na Wananchi kuhusu changamoto ya barabara kukatika haswa katika kipindi hiki cha mvua. Toeni maelekezo ya jumla kwa TARURA nchi nzima ili barabara zinazosimamiwa na TARURA na hazipitiki wakazitazame ili Wananchi waweze kupata huduma,” ameagiza Spika.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa TAMISEMI David Silinde amesema ”Nawaagiza Mameneja wote wa Mikoa wa TARURA pamoja na Halmashauri zote nchini kuanzia siku ya kesho [leo] waende wakafanye tathmini ya haraka iwezekanavyo na kutupatia Ofisi ya TAMISEMI ili tuweze kupeleka fedha za dharura kuhakikisha kazi inafanyika”
Silinde ameongeza kwamba agizo hilo watatekelezeka na kupeleka taarifa ndani ya Bunge kabla ya mkutano wa sita wa Bunge la 12 haujaisha.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya amewaagiza mameneja wa TANROAD nchini kukagua barabara ambazo hazipitiki na kuzifanyia matengenezo, na kama watahitaji msaada wa makao makuu watoe taarifa.