WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema wanasiasa na baadhi ya wananchi wanaobeza juhudi au miradi inayotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan hawajui watendalo, huku akiwafananisha na mashabiki.
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Badala yake amewasihi Watanzania wanaomlaumu wamvumilie kwa kuwa Rais Samia ana nia njema ya kuuinua uchumi.
Alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mamia ya wakazi wa Mkoa wa Manyara waliojitokeza katika maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema Rais yeyote anapoingia madarakani mwanzoni huwa ni shida na hukumbana vikwazo kadha wa kadha.
"Tuache ushabiki, Rais ana nia njema, atatupeleka mahali panapotakiwa na uchumi wetu utakua," alisema Sumaye.
Aidha, alisema kitu anachokifanya Rais Samia kwa sasa anataka kujenga ukuta wa uchumi wenye nguvu zaidi.
Sumaye, alisitiza kuwa nchi ina mambo mengi na yote hayawezi kuwa kipaumbele, hivyo anashauri ni vyema wananchi wanaomlaumu, wampe nafasi ili alifikishe Taifa mahali pazuri.
Kuhusu katiba mpya, Sumaye, alisema watu wanaong'ang'ana na kupaza sauti za kutaka katiba mpya, hawana nia ya kuijenga nchi zaidi ya maslahi binafsi ya kiutawala.
Alisema hakuna mtu asiyetaka katiba mpya, ila wamuache kwanza Rais kama alivyoomba muda ili ajenge uchumi wa nchi.
"Katiba mpya muda wake haujafika, katiba haiwezi kumzuia mtu mjeuri, hivyo hata akiingia mtu mwingine tukiwa na katiba anaweza asifanye baadhi ya mambo," alisisitiza Sumaye.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere, akitoa salamu za serikali, alisema serikali itaendelea kusimamia ilani ya CCM kwa mambo ambayo yameainishwa na mazuri ambayo hayajaainishwa kwenye ilani.
Alisema mkoa, unajenga mji wa kibiashara wa madini wa Mirerani ulioko Wilaya ya Simanjiro ili kuinua uchumi wa wachimbaji, ingawa haujatajwa kwenye ilani.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Manyara, Naomi Kapambala, alisema wakati wa kuelekea maadhimisho hayo, tayari wamesajili wanachama wapya 1,426 na kufikisha idadi ya wanachama 400,000 waliosajiliwa rasmi mpaka sasa.